Mkuu wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro akizungumza katika hafla ya kukabidhi magari manne kwa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoani Kigoma ikiwa sehemu ya mkakati wa serikali ya kuimarisha utendaji kazi wa vikosi hivyo.
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Balozi amekabidhi gari la kuzimia moto na uokoaji kwa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa Kigoma huku akitoa wito kwa wananchi na taasisi zote mkoani humo kulitumia gari hilo kwa ajili ya kukabiliana na majanga mbalimbali yatakayotokea mkoani humo.
Balozi Sirro alisema hayo akikabidhi gari hilo kwa uongozi wa kikozi cha zimamoto na uokoaji mkoa Kigoma akitanabaisha kuwa serikali imejipanga kuhakikisha idara na mamlaka zake mbalimbali zinakuwa na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.
Gari la kuzima moto (kushoto) na gari la kubeba maji (boza - kulia) ambayo ni miongoni mwa gari nne zilizokabidhiwa kwa kikosi cha Zimamoto mkoani KigomaMkuu huyo wa mkoa alisema kuwa anataraji uwepo wa gari hilo itakuwa chachu kubwa katika kukabili na majanga ya moto na majanga mbalimbali yatakayotokea mkoani humo ambapo gari hilo linaongeza nguvu katika magari yaliyokuwepo awali katika idara nyingine ikiwemo Uwanja wa ndege wa Kigoma na Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji.
Pamoja na gari hilo la kuzima moto pia kikosi hicho cha zimamoto na uokoaji mkoa Kigoma kimekabidhiwa gari moja la kubeba maji (Boza), gari ya kubebea wagonjwa na majeruhi (Ambulance) na gari moja kwa ajili ya matumizi ya utawala ambapo Mkuu wa mkoa Kigoma ametaka magari hayo kutumika vizuri kwa makusudio yaliyoelekezwa.
Awali Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na uokoaji mkoa Kigoma, Michael Maganga alisema kuwa kikosi hicho kimekabidhiwa jumla ya magari manne ikiwemo gari la zimamoto, gari moja la kubeba maji (Boza), gari ya kubebea wagonjwa na majeruhi (Ambulance) na gari moja kwa ajili ya matumizi ya utawala na operesheni ikiwa ni kuimarisha utoaji huduma mkoani humo.





0 Comments