Header Ads Widget

SERIKALI YAKABIDHI PIKIPIKI KUSAIDIA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KAGERA.

 

Na Shemsa Mussa -Matukio Daima 

Kagera.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amos Mpanju, amekabidhi pikipiki tisa (9) kwa halmashauri za Bukoba, Missenyi, na Ngara mkoani Kagera, zitakazotumika kuwawezesha maafisa maendeleo ya jamii kufika kwa urahisi zaidi katika maeneo ya vijijini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mpanju alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha huduma za maendeleo zinawafikia wananchi hadi ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa na kata.

> “Division za maendeleo ya jamii zina jukumu la kufanya kazi pamoja katika kusikiliza, kuelimisha, na kusaidia wananchi kuwa na maendeleo yao wenyewe,” alisema Mpanju.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana pale wananchi wanaposhiriki kikamilifu katika miradi ya serikali na kujiona kuwa sehemu ya wamiliki wa huduma zinazotolewa.

> “Nyie ni wataalamu wenye mbinu za kuwaonyesha wananchi namna ya kushiriki miradi na kunufaika nayo, ili waone huduma hizo ni zao na waweze kukimbilia fursa za kujiletea maendeleo,” ameongeza.

Mpanju pia amewataka wananchi kutumia fursa hizo kuacha kupoteza muda kwenye maeneo yasiyo na tija kama vilabu, badala yake wajikite katika shughuli za kiuchumi zinazoweza kuboresha maisha yao.

Aidha, alibainisha kuwa kuna rasilimali nyingi zinazowazunguka wananchi, lakini wengi hawazitumii ipasavyo kwa sababu hawana elimu ya kuzitambua na kuzitendea kazi. Alisema maafisa maendeleo ya jamii watatumia usafiri huo mpya kuwasogelea wananchi na kuwapatia elimu hiyo muhimu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI