Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Kiongozi wa chama Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amemtaka mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya CCM Peter Serukamba kustaafu siasa kwani zama za kupata ubunge kwa nguvu ya pesa zimeisha na badala yake nguvu ya umma itaamua kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Kabwe alisema hayo katika viwanja vya soko la Mwandiga halmashauri ya wilaya Kigoma mkoani Kigoma wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma kaskazini kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Kiza Mayeye.
Kiongozi wa chama mstaafu ACT Wazalendo Zitto Kabwe ( kushoto) akimtambulisha kwa wananchi mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma Kiza Mayeye wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge za jimbo hilo zilizofanyika katika viwanja vya soko la Mwandiga wilaya ya Kigoma Agosti 8 mwaka huu
Kiongozi huyo wa Chama Mstaafu alisema kuwa chama hicho kimemsimamisha Kiza Mayeye kuwa mgombea ubunge jimbo la Kigoma Kaskazini kwa sababu kimeona ana sifa, ana uthubutu na uwezo wa kuwasimamia na kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo na kwamba siyo kila wakati nguvu ya fedha inaweza kuamua mgombea kuwa kiongozi hata kama wananchi hawamkubali.
Akizungumza katika mkutano huo Mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Kiza Mayeye alisema kuwa anakuja na vipaumbele vitano ambavyo atavisimamia katika kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja upatikanaji wa huduma bora za afya ikiwemo huduma za kujifungua wajawazito na yupo tayari kutumia mshahara wake kununua vitanda vya kujifungulia sambamba na kuwepo kwa elimu bora ambayo kila mwananchi atamudu gharama ambayo ataitumia kutengeneza maisha yake.
Mgombea huyo amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama karibu na makazi ya watu, uboreshaji wa miundo mbinu ya barabara kwenda kwenye maeneo ya uchumi na kilimo huku suala la uwezeshaji na kuweka mazingira mazuri kwa vijana na wanawake ikiwa moja ya mambo atakayoyabeba kwa uzito mkubwa.
Sehemu ya Wanachama na wapenzi wa chama cha ACT Wazalendo waliohudhuria uzinduzi wa kampeni za ubunge za jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani zilizofanyika katika viwanja vya soko la Mwandiga wilaya ya Kigoma ambapo ACT Wazalendo imemsimamisha Kiza Mayeye
Akihitimisha mkutano wake huo wa uzinduzi Mgombea huyo alisema kuwa mwaka 2020 aligombea na kupata kura nyingi lakini hakutangazwa na kwamba amewaomba wasimamizi wa uchaguzi kutenda haki kwa kumtangaza mshindi halali kwa kufanya uchaguzi huru na haki.
0 Comments