Na COSTANTINE MATHIAS, Kigoma.
WAKULIMA wa pamba katika kijiji cha Kanyonza, wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma wameeleza namna zao hilo limewanufaisha kiuchumi, huku wakihimiza kupatiwa pembejeo kwa wakati ili kuongeza uzalishaji.
Erick James, mkazi wa Kijiji hicho amesema tangu mwaka 2019/20 ameweza kununua kiwanja na kujenga nyumba kupitia mapato ya pamba na kueleza kuwa zao hilo limeonyesha kumwinua kiuchumi
“Nataka kuongeza uzalishaji kwa kulima pamba kisasa na kwa kuzingatia kanuni za kilimo, tunaomba serikali kupitia Bodi ya Pamba ituletee Pembejeo za Pamba mapema” amesema.
Nicholas James kutoka Kijiji cha Mganza amesema mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT) umewasaidia wakulima kuongeza tija, lakini naye akasisitiza umuhimu wa kupata mbegu na mbolea mapema ili wapande kwa wakati.
Bernadeta Alfred na Alfred Elias nao wanasema wamefanikiwa kujenga nyumba na kusomesha watoto kupitia pamba, wakisisitiza serikali iwawezeshe kupata pembejeo na dawa mapema.
Afisa wa BBT, Zebedayo Daniel, amesema wakulima sasa wamepiga hatua kutoka kuzalisha kilo 150 hadi 600 kwa ekari, kutokana na elimu wanayopata toka kwa wataalamu hao.
"Tunawahimiza kutumia mbolea na kufuata kanuni ili kuongeza mavuno, ikiwemo kupanda kwa nafasi na kwa wakati,” alieleza.
Wakulima hao wana imani uzalishaji utaongezeka zaidi endapo changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi.
Mwisho.
0 Comments