Rais wa Marekani Donald Trump amesema siku ya Jumatatu kuwa hakujulishwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mapema kuhusu shambulizi la Israel nchini Qatar wiki iliyopita.
Maoni ya Trump yanatolewa baada ya ripoti ya Axios kusema kuwa Netanyahu alimfahamisha rais wa Marekani kuhusu shambulizi hilo muda mfupi kabla ya kutokea.
Utawala wa Trump umesema uliarifiwa tu baada ya makombora kurushwa angani, na hivyo kumnyima Trump fursa ya kupinga shambulizi hilo.
Axios iliripoti, ikiwanukuu maafisa wa Israeli, kwamba Ikulu ya Marekani ilijua mapema, hata ikiwa muda wa kusitisha shambulizi hilo ulikuwa kidogo.
Israel ilifanya shambulizi la kujaribu kuwaua viongozi wa kisiasa wa Hamas kwa shambulizi la anga nchini Qatar siku ya Jumanne, na kuzidisha hatua yake ya kijeshi Mashariki ya Kati.
Shambulizi hilo lilishutumiwa pakubwa Mashariki ya Kati na kwingineko kama kitendo ambacho kinaweza kuzidisha hali ya wasiwasi katika eneo ambalo tayari linakumbana na changamoto zake.
Awali, Trump alisema hakuhusika katika uamuzi wa Israel kuivamia Qatar.
Alipoulizwa siku ya Jumatatu ikiwa Netanyahu alizungumza naye moja kwa moja kumtahadharisha kuwa Israel itavamia viongozi wa Hamas nchini Qatar, "Hapana, hapana, hawakunijulisha," Trump alisema.
Ofisi ya Netanyahu ilisisitiza baada ya Axios kuripoti kwamba shambulizi hilo lilikuwa operesheni "huru kabisa" ya Israeli.
0 Comments