
Na COSTANTINE MATHIAS, Singida.
WAKULIMA wa Pamba kwenye Halmashauri za wilaya za Iramba, Ikungi, Manyoni, Mkalama na Singida Mkoani Singida wametakiwa kung'oa na kuchoma moto ya Pamba masalia na kuandaa mashamba ya Kilimo cha zao hilo kwa kuzingatia kalenda ya Kilimo cha pamba.
Aidha wakulima hao wametakiwa kuzingatia Elimu wanayopewa na Maafisa Ugani kupitia Mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ili waweze kuzalisha kwa tija na kujiinua kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa Habari za Pamba, Mkaguzi wa Pamba kutoka Bodi ya Pamba (TCB), Mkoa wa Singida, Abdlahaman Sempule amesema kuwa wanashirikiana na Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhamasisha Kilimo cha pamba kwa Wakulima.
"Tunashirikiana na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha wakulima wanapata Elimu na kuhamasisha kulima kisasa ili kuongeza tija, kwa sasa tunatoka elimu kupitia wakulima viongozi kukata au kung'oa masalia ya Pamba ili kudhibiti Wadudu wanaohama toka msimu mmoja kwenda mwingine" amesema.
Steven Disa, mkulima wa pamba kutoka kijiji Matumbo kata ya Makulo, wilaya ya Singida amesema kutokana na kuzingatia kanuni za kilimo cha pamba ameweza kuzalisha kilo 1000 kwa ekari moja katika msimu 2024/2025 ambazo zimempatia fedha za kujikwamua kiuchumi.
"Nilianza kulima Pamba ekari mwaka 2022 kwa majaribio, nilianza kulima nikiwa pekee yangu Kijijini hapa, nilipata Kilo 660 nikauza na kulipa ada za wanafunzi, mwaka jana nilipata 900 eneo hilo hilo, na 2025 nimelima kwa tija na kupata kilo 1000 nimeuza kwa bei ya shilingi 1150." Amesema Disa.
Daud Mande, mkulima wa Kijiji cha Matumbo wilaya ya singida vijiji amesema alihamasika kulima Pamba baada ya kuona mkulima mwenzake (Disa) akinufaika na Kilimo cha pamba.
Amesema alishawishika kulima Pamba na kuzalisha Kilo 360 na mara ya pili (2025) alizalisha kilo 780 kwa ekari moja huku akiahidi kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa Kilimo cha pamba.
Mwisho.
0 Comments