Na. Mwandishi Wetu, Dar.
WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wapo katika hatua za kuanza ujenzi wa daraja refu litakalojengwa kwa mawe eneo la Mwanagati -Magole katika Mto Mzinga, Temeke, Dar es salaam.
Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa Teknolojia Mbadala TARURA – Makao Makuu Mhandisi Mshauri Pharels Ngeleja mbele ya Waandishi wa habari kando ya Mkutano mkuu wa mwaka wa Wahandisi Septemba 26, 2025, katika ukumbi wa mikutano Mlimani City Dar es salaam.
Muhandisi Ngeleja amebainisha kuwa, Daraja la Mwanagati limepangwa kujengwa kwa teknolojia hiyo ya mawe na litakuwa la kipekee kwa Dar es salaam kwani ndo litakuwa refu kuliko yote hapa nchini.
"Neno daraja ni uchumi, ili barabara iwe inapitika lazima iwe na daraja. Sisi kama TARURA tumeweka umuhim mkubwa katika madaraja kwani hadi sasa madaraja 453 yamejengwa kwa gharama nafuu kabisa." Amesema Mhandisi Ngeleja.
Na kuongeza kuwa: "Wananchi wa mwanagati kwa sasa wanatumia daraja la kuvuko ambalo ni la mbao na wanapita kwa shida, hivyo litakapokamilika litakuwa msaada mkubwa sana kwa Wananchi wa maeneo hayo na jirani katika Wilaya ya Temeke.
Muhandisi Ngeleja amesema Madaraja haya ya mawe sio kwamba yanajengwa Tanzania, ni kwamba teknolojia hiyo ipo miaka mingi nchi za Ulaya na duniani kote.
"Kwa Tanzania TARURA tunaendelea na ujenzi wa madaraja haya ya mawe, miaka na miaka hata huko Ulaya wanatumia.
Haya madaraja ni imara kuliko yale ya zege, hata reli yetu inayoenda Arusha na ile ya Kati baadhi ya madaraja yake yamejengwa kwa mawe, Ile reli Ina miaka zaidi 100 na bado mnaona yapo vizuri.
TARURA imekuwa ikiendelea na miradi ikiwemo ya barabara na madaraja katika Mikoa mbali mbali ikiwemo Mwanza, Kigoma, Rukwa, Morogoro. Ambapo barabara za mawe zimeweza kurahisisha Wananchi katika shughuli zao za kiuchumi.
"Tumeweka nguvu kwenye ujenzi huu, ujenzi huu umekuwa ukifanyika katika maeneo yote ya Tanzania nzima". Amemalizia Mhandisi Ngeleja.
![]() |
Msimamizi wa Teknolojia Mbadala TARURA – Makao Makuu Mhandisi Mshauri Pharels Ngeleja akizungumza mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani) kando ya Mkutano mkuu wa mwaka wa Wahandisi 2025, katika ukumbi wa mikutano Mlimani City Dar es salaam. |
0 Comments