Na COSTANTINE MATHIAS, Igunga.
WAKULIMA wa Pamba katika kijiji cha Mbutu, kata ya Mbutu wilayani Igunga, wamepata suluhisho la kipekee la kuongeza tija kwenye kilimo cha pamba kupitia mbolea ya mkaa inayotokana na masalia ya miti ya pamba.
Mbinu hii mpya, inayojulikana kitaalamu kama Bio Char, imeanza kuleta mwitikio chanya kwa wakulima na kutoa matumaini ya mavuno bora na kipato cha ziada.
Lucas Masunga Sita, mkazi wa Mbutu, ameeleza faida kubwa zinazopatikana kupitia ubunifu huu na kusema kuwa Masalia au miti ya pamba inapatikana kwenye mazingira yao.
"Haya ni mabaki ambayo awali tuliyachukulia kama taka, lakini sasa tumegundua yana thamani kubwa, Mbolea hii haina gharama, inaleta rutuba na kutupa mavuno mazuri. kwa kweli hii ni faida kubwa kwa mkulima,” anasema.
Anaongeza kuwa moja ya kanuni muhimu za kilimo cha pamba ni kuhakikisha masalia hayaondoki mashambani na kwamba kupitia programu za uhamasishaji zinazofanywa na wakulima wawezeshaji wanaopita vijijini, elimu imetolewa juu ya umuhimu wa kuondoa masalia haya na kuyageuza bidhaa zenye manufaa.
“Wakulima wanaoacha masalia mashambani bila kuyachoma au kuyatumia ipasavyo, mara nyingi huishia kupata mavuno duni. Sasa tunajua njia bora ya kuyatumia kwa faida yetu,” anasisitiza Lucas.
Afisa Kilimo wa BBT (Building a Better Tomorrow), Kijiji cha Mbutu, Nice Thomas, anasema kuwa baada ya mavuno ya pamba kumalizika, masalia ya miti na mabaki ya mashambani yamekuwa yakionekana kama taka isiyo na faida.
Anasema kuwa kupitia elimu na uhamasishaji, sasa masalia hayo yanachomwa kwa njia maalumu na kutengeneza mbolea hai ambayo haina gharama wala madhara kwa jamii na mazingira.
"Mbolea ya mkaa si tu kwamba haina gharama, bali pia husaidia kuhifadhi unyevunyevu kwenye udongo. Ina chembechembe (particles) maalum zinazotunza maji na kuendeleza viumbe hai vya ardhini, hii inasaidia sana kuongoza ratiba za ukuaji wa mimea shambani,” anaeleza Nice Thomas.
Moja ya changamoto kubwa inayowakumba wakulima wa pamba katika maeneo mengi ya Igunga ni udongo wenye chumvichumvi unaopunguza rutuba na kuathiri mavuno ambapo kupitia matumizi ya mbolea ya mkaa, hali hiyo sasa imeanza kudhibitiwa.
Mbolea hii inaimarisha rutuba kwa kuboresha muundo wa udongo, kupunguza asidi na kuongeza upatikanaji wa virutubisho. Wakulima wanasema kuwa udongo ambao awali ulikuwa mgumu na usioweza kustawisha mimea, sasa unaonyesha mwitikio mzuri baada ya kutumia mbolea ya mkaa.
Zaidi ya hayo, wakulima wanaona faida ya kiuchumi kwani mkaa unaotokana na masalia unaweza pia kutumika kama nishati mbadala ya kupikia majumbani na njia ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa wa mafiga.
Mbolea ya mkaa haina tu faida kwa wakulima, bali pia inachangia katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa ina uwezo wa kuhifadhi kaboni ardhini kwa muda mrefu, inasaidia kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa (carbon emissions) kwenye anga.
Mwisho.
0 Comments