Na COSTANTINE MATHIAS, Igunga.
SERIKALI wilayani Igunga Mkoani Tabora imewachukulia hatua viongozi wa vyama 32 vya Ushirika (Amcos), ikiwemo kufikishwa Mahakamani kwa makosa ya kuchezea mizani ya pamba kwa lengo la kuwaibia wakulima wa.
Akiongea na waandishi wa Habari za Pamba, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sauda Mtondoo amesema kuwa viongozi wa vyama hivyo wakiwemo Wenyeviti na Makatibu wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
"Suala la kuchezea mizani lilijitokeza katika wilaya yetu ya Igunga, hatua zilichukuliwa kwenye vyama 32, Wenyeviti na Makatibu walikamatwa na hatua zaidi zinaendelea za kuwafikishia mahakamani" amesema.
Amesema kuwa katika msimu uliopita, wilaya hiyo ilishika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa Pamba Kitaifa kwa kuzalisha tani Milioni 26 na kwamba wanaendelea kutoa hamasa kwa Wakulima ili kulipa kipaumbele zao hilo la kibiashara.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa eneo hilo ni kitalu cha uzalishaji wa mbegu, hivyo linapaswa kutunzwa na kwamba Wananchi wanaelimishwa ili kuzalisha Pamba mbegu ambayo itatumika kwa wakulima wengine wa Pamba.
Ameeleza kuwa hadi sasa wilayani hiyo imekusanya kiasi cha tani Milioni 25 za Pamba na kwamba wanaendelea kuelimisha wakulima kuandaa mashamba ikiwemo kung'oa masalia kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa kilimo 2025/2026.
"Tunahamasisha ung'oaji wa masalia ya Pamba ili kudhibiti Wadudu, hadi sasa asilimia 60 ya maotea yameshang'olewa na kuchoma...tunashirikia na Maafisa Ugani kutoa elimu na maandalizi kwa ajili ya msimu wa kilimo ujao yameshaanza ikiwemo mgao wa mbegu tani 1660 na tayari tani 890 zimesambazwa" amesema.
Mwisho.
0 Comments