Israel imetekeleza mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa Yemen, Sanaa, siku ya Alhamisi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vinavyohusiana na Wahouthi pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Israel.
Mashambulizi hayo yamesababisha vifo na majeruhi kadhaa.
Mashambulizi hayo yanakuja siku moja baada ya watu kadhaa kujeruhiwa katika mji wa Eilat, Israel, siku ya Jumatano, kufuatia shambulizi la ndege zisizo tumia rubani lililodaiwa na kundi la Wahouthi.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imeripoti kuwa Benjamin Netanyahu ndiye aliyeagiza shambulizi hilo dhidi ya Yemen siku ya Alhamisi, wakati akiwa safarini kuelekea New York.
Ofisi hiyo iliongeza kuwa Netanyahu alikuwa akipokea taarifa za moja kwa moja kuhusu operesheni hiyo kutoka kwa Waziri wake wa Ulinzi, Mkuu wa Majeshi, na Katibu wake wa Kijeshi.
Baadaye, kundi la Houthi Ansar Allah nchini Yemen lilitangaza kuzindua kombora la kisasa la kasi kubwa linaloitwa Palestine 2 kuelekea Israel, wakidai kuwa kombora hilo limesababisha kusitishwa kwa shughuli katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion.
Televisheni ya Al Masirah, inayohusiana na Wahouthi, ilinukuu chanzo kutoka Idara ya Usalama na Ujasusi kikisema kuwa “uvamizi wa Israel dhidi ya Sanaa ulilengwa katika kituo cha marekebisho ya tabia (gereza) kinachosimamiwa na idara hiyo, ambacho kinahifadhi wafungwa na mahabusu.”
Hapo awali, kituo hicho cha habari kiliripoti kuhusu “uvamizi wa Israel unaolenga mji mkuu Sanaa,” uliotokea wakati huo huo na matangazo ya hotuba ya kila wiki ya kiongozi wa Wahouthi, Abdulmalik al-Houthi.
Mwandishi wa shirika la habari la AFP aliyepo Sanaa aliripoti kusikia milipuko mikubwa na kuona moshi ukipanda kutoka maeneo matatu tofauti ya jiji hilo.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yisrael Katz, alituma ujumbe kupitia mtandao wa kijamii X akirejea tishio lake kwa Wahouthi, akisema: “Wahouthi, magaidi wa Yemen, wamekataa kujifunza kutoka Iran, Lebanon na Gaza sasa watalazimika kujifunza kwa njia ngumu.”
Aidha, alisisitiza kwamba, “yeyote anayehujumu Israel, atajibiwa kwa nguvu mara saba zaidi.”
Kwa upande wake, Meya wa Eilat, Eli Lankri, katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha 12 nchini Israel, alitoa wito wa “mashambulizi makali dhidi ya Wahouthi,” akibainisha kuwa “mashambulizi yao ya mara kwa mara yamevuruga shughuli katika bandari ya Eilat.”
Mwisho wa mwezi Agosti, shambulizi la anga la Israel lilimuua Waziri Mkuu wa Wahouthi, Ahmed Ghaleb al-Rahwi, pamoja na mawaziri na maafisa wengine tisa waliokuwa kwenye kikao mjini Sanaa.
Mapema mwezi Septemba, watu wasiopungua 46 waliuawa katika mashambulizi ya Israel yaliyolenga mji mkuu wa Yemen, Sanaa, na mkoa wa kaskazini wa Al-Jawf wakiwemo watu 38 waliouawa Sanaa ambapo vituo vya habari na taasisi zinazohusiana na Wahouthi vililengwa.
0 Comments