Header Ads Widget

TAASISI ZA ELIMU GEITA ZATAKIWA KUANZISHA PROGRAMU YA MAZIWA SHULENI

 


Na Matukio Daima Media Geita

MKUU wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba amezitaka taasisi za elimu mkoani Geita kuanzisha programu maalumu ya utoaji maziwa katika taasisi  hizo kama ilivyo programu ya lishe shuleni ili kuongeza kasi ya unywaji wa maziwa.


Ametoa agizo hilo leo Septemba 24, 2025 wakati akitoa hotuba ya kuhitimisha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya Unywaji Maziwa Shuleni akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela huku amewataka Maofisa Elimu wa Mkoa huo kujipanga ili kuona namna watakavyotekeleza Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni kama ilivyo kwenye Mpango wa Lishe ili kuendelea kujenga afya za wanafunzi.


Vilevile ametoa rai kwa wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kuhakikisha maziwa yanapatikana katika famiilia ili kuendeleza utamaduni wa unywaji wa maziwa.


Mwakilishi wa Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Deorinidei Mng'ong'o ameeleza kuwa jumla ya lita 240 za maziwa zimegaiwa kwa wanafunzi wenye uhitaji maalumu walioko mkoani Geita huku wanafunzi wapatao 300 kutoka katika vituo vya kulelea yatima mkoani humo wakinufaika na mpango huu.


Bodi ya Maziwa Tanzania chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kufikia mikoa 11 nchini ili kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni ambapo shule 218 zimefikiwa huku takribani wanafunzi 120,000 wakifikiwa na programu hii.


Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Unywaji  Maziwa Shuleni yaliyofikia kilele mkoani Geita yakiwa na lengo la kuhamasisha Unywaji wa Maziwa Shuleni yamesindikizwa na kauli mbiu isemayo  Kwa Matokeo Mazuri Shuleni na Afya Bora Maziwa ndio Mpango Mzima.


Mwisho....

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI