Mara ya kwanza aliposhika viatu vya riadha akiwa kijana mdogo huko Singida, hakuwahi kudhani kwamba baada ya miaka miwili baadaye angekuwa shujaa wa taifa lake na bara la Afrika.
Septemba 15, 2025, Alphonce Felix Simbu ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya riadha ya dunia.
Miaka minane iliyopita, katika mahojiano na BBC akieleza ndoto zake baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki mashindano ya dunia, Simbu alisema kwa kujiamini: "naiona dhahabu itakuja." Sasa kauli hiyo imekuwa unabii uliotimia, baada ya ushindi wa Tokyo 2025.
"Sikuwa najua ningeshinda, lakini nilipoona kwenye skrini ya TV uwanjani kwamba mstari wa kumaliza hauko mbali, nikasema uuh nikazane! Nashukuru nimetengeneza historia, hakuna Mtanzania aliyewahi kushinda medali ya dhahabu", anasema Simbu baada ya kuweka historia.
KUTOKA MAMPANDO MPAKA BINGWA WA DUNIA
Simbu aliposhinda medali ya fedha huko Birmingham mwaka 2022
Simbu aliyezaliwa tarehe 14 Februari 1992 wilayani Ikungi, mkoa wa Singida, alianza riadha akiwa shule ya msingi kwa kujifurahisha na kwa mapenzi kama ilivyo kwa wanamichezo wengine akifanya mazoezi ya kawaida na marafiki zake.
Alipokumbuka hatua zake za mwanzo, Simbu aliwahi kueleza:
"Tulikua tunafanya mazoezi tu tukisikia kuna mashindano fulani, yakiisha nasi tunaacha mazoezi."
Akiwa anasoma katika shule ya Msingi Mampando, Wilaya ya Ikungi, Singida, mwalimu wake wa muda mrefu, Madai Jambau, aliona uwezo na kipaji chake, akaaamua kumshawishi akifanyie kazi.
Akamchukua na kuanza kumfundisha riadha kwa mazoezi maalumu kwenye shule ya msingi Lighwa, huko huko Ikungi kabla ya kuhitimu.
Alipokuwa Shule ya Sekondari ya Winning Spirit, alianza kujikita zaidi kwenye mbio ndefu, hasa baada ya masuala ya matokeo ya mitihani kutokwenda vizuri. Hapo ndipo alipoamua kujiingiza rasmi kwenye marathon.
Lakini mwaka 2015, akawa na uamuzi wa kubadilisha hatma yake.
"Nakumbuka mwaka 2015, kulikuwa na mashindano ya dunia yanafanyika Beijing, nikiwa kambini Mbulu, nikaamua na kumwambia kocha nataka kufanya marathon ya majaribio ili nifuzu mashindano ya dunia. Kocha alinikubaliana, nilifanya mazoezi kuanzia mwezi wa tano hadi wa saba, nikashiriki mashindano ya Gold Coast Airport Marathon tarehe 5 Julai 2015. Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kukimbia marathon, nikafanikiwa kufikia kiwango kwa kukimbia saa 2:12:01."
HAPO SAFARI YA KIMATAIFA IKAANZA RASMI
Baada ya kufuzu, alishiriki mashindano ya dunia Beijing 2015, kisha akaenda kwenye Olimpiki Rio 2016, akimaliza nafasi ya tano kwenye marathon. Mwaka 2017 ukawa wa kumbukumbu nzuri zaidi kwake, alishinda Mumbai Marathon Januari na kisha akatwaa medali ya shaba kwenye Mashindano ya dunia London, akimaliza kwa muda wa saa 2:09:51. Akaanza kufahamika nyumbani Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla
Baadaye alimaliza nafasi ya 16 kwenye Mashindano ya dunia Doha 2019, kisha nafasi ya saba kwenye Olimpiki Tokyo 2021. Mwaka 2022, akatwaa medali ya fedha kwenye mashindano ya Jumuia ya madola (Commonwealth Games) huko Birmingham, Uingereza.
Mwishoni mwa mwaka 2024, aliboresha rekodi yake binafsi kwa kukimbia Valencia Marathon kwa muda wa saa 2:04:38, na mwaka 2025 akamaliza wa pili kwenye Boston Marathon kwa saa 2:05:04.
DHAHABU YA KIHISTORIA TOKYO 2025
Simbu (kushoto) akimaliza mbio za dunia za Tokyo, 2025 mbele ya mpinzani wake wa karibu Amanal Petros kutoka Ujerumani
Septemba 15, 2025, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Tokyo, Simbu aliibuka mshindi wa marathon ya Mashindano ya Dunia, akimaliza kwa muda wa saa 2:09:48.
Baada ya ushindi huo, alisema, "Najisikia vizuri, kwenye mstari wa kumaliza nilikuwa nimechoka kweli lakini nilikuwa na furaha. Ilikuwa mbio ngumu kwa sababu kila mtu alikuwa na nguvu barabarani, nafikiri kila mtu alijiandaa vyema."
Simbu anaeleza kuwa sehemu ya mwisho ya kumaliza mbio hizo za kihistoria kwake ilikuwa ngumu zaidi:
"Tulivyokuwa tunakaribia kuingia uwanjani, tulikuwa kama kundi. Ilikuwa ngumu, lakini kichwani mwangu nilijisemea, nikiingia uwanjani, kwenye mstari wa kumaliza, nitajaribu… kweli nikafanikiwa", anaeleza na kuongeza kuwa alipokuwa anaingia uwanjani kidogo apotee njia, "Nilidhani upande wa maafisa ndo sahihi, lakini nikawaona wenzangu wanakata kulia, nikasema 'aha…' nilishikwa na butwaa."
Ushindi huu umeonekana pia kama zawadi kwa wale waliomlea na kumfunza tangu mwanzo. BBC ilizungumza na Madai Jambau, mwalimu wake wa muda mrefu. Kwa sauti ya furaha, alisema:
"Nafuraha sana, nilikuwa namuamsha (Simbu) usiku usiku na wenzake kufanya mazoezi. Leo naona matunda yake."
TAKWIMU NA ALAMA YA SIMBU
Kwa zaidi ya muongo mmoja, Simbu amekuwa sura ya riadha ya Tanzania, akishiriki mashindano makubwa ya dunia ikiwemo Olimpiki, Jumuia ya madola, na mashindano ya dunia. Rekodi yake binafsi ni 2:04:38 aliyoiweka Valencia 2024, muda unaomuweka miongoni mwa wakimbiaji wa kasi zaidi duniani.
Kwa mujibu Shirikisho la riadha la dunia, Simbu ni mmoja wa wakimbiaji wa bora wa mbio ndefu (marathon), akishika nafasi ya 16 kwa ubora duniani. Amefanikiwa kutwaa medali ya dhahabu na shaba katika mashindano ya dunia. Aidha, ameibuka na medali ya fedha mara mbili katika michezo ya Jumuia ya madola. Katika mashindano ya Olimpiki, Simbu amekuwa miongoni mwa wakimbiaji wa ngazi ya juu, akimaliza katika nanae bora mara mbili. Mafanikio haya yote yanaonyesha uwezo wake mkubwa na uvumilivu katika mbio ndefu.
Lakini zaidi ya takwimu, Simbu sasa ni alama ya matumaini mapya kwa taifa. Ushindi wake wa dhahabu Tokyo 2025 umetimiza ndoto alizozitamka miaka ya nyuma kwa BBC: "naiona dhahabu itakuja." Na leo, ndoto hiyo imekuwa kweli.
0 Comments