Header Ads Widget

SABA MATATANI,WAKIWEMO ASKARI POLISI WAWILI KWA WIZI WA MBOLEA YA MILIONI 45.

 

Na Moses Ng'wat, Songwe.

Jeshi la Polisi mkoani Songwe linawashikilia watu saba, wakiwemo askari polisi wawili, kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mifuko 534 ya mbolea aina ya UREA yenye thamani ya Shilingi milioni 45,454,080.

Mbolea hiyo, mali ya kampuni ya Ocean Network ya nchini Zambia, ilikuwa inasafirishwa kwa njia ya reli kutoka Dar es Salaam kuelekea nchi jirani ya Zambia, kabla ya kuibwa usiku wa Agosti 19, 2025 katika Kijiji cha Nanyala, Wilaya ya Mbozi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, akizungumza na waandishi wa habari Septemba 2, 2025, alieleza kuwa watuhumiwa hao walishirikiana kwa kupanga njama na kusimamisha treni yenye usajili wa namba 0139A mali ya TAZARA, katika eneo lisilo rasmi kwa ajili ya kushusha mbolea hiyo.

Alisema kuwa watuhumiwa hao ni pamoja na madereva wa treni na wafanyabiashara wa mbolea, huku askari wawili waliokuwa wakisindikiza treni hiyo nao wakihusishwa moja kwa moja na tukio hilo

Hata hivyo, Kamanda Senga hakuwa tayari kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa sababu za kipelelezi.

Aliongeza kuwa, katika msako uliofanyika, Polisi walifanikiwa kukamata mifuko 134 ya mbolea hiyo kwenye nyumba ya mmoja wa watuhumiwa katika Kijiji cha Ipoloti, Kata ya Bara, Wilaya ya Mbozi.

Kamanda Senga alisema uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini wahusika wengine na magari yaliyotumika kubeba mbolea hiyo, akisisitiza kuwa wote waliohusika watakabiliwa na mkono wa sheria.

“Hili ni tukio la kihalifu linalohusisha mtandao mpana wa watu hivyo tunafanya uchunguzi wa kina na tutahakikisha wote waliohusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Kamanda Senga.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI