Header Ads Widget

POLISI MBEYA WAMTIA MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA MTOTO (15)

 


Na Matukio Daima Media, Mbeya 

Polisi mkoani Mbeya inamshikilia mtu mmoja Magreth Jonas Lyanda, mkazi wa mtaa wa Mwenge wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kwa tuhuma za mauaji ya mtoto mwenye umri wa miaka 15 aitwaye Rehema Sikalengo aliyekuwa akiishi katika eneo la DDC mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi wilayani Mbeya.


Akitoa taarifa kwa vyombo habari, kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi SACP Benjamin Kuzaga, amesema mnamo tarehe 16 Septemba, 2025 huko eneo la DDC Mbalizi, Kata ya Utengule Usongwe katika Mbalizi mtoto Rehema Sikalengo [15] alikutwa ameuawa nyumbani kwao jikoni na mwili wake ukiwa umetumbukizwa ndani ya Jaba lililokuwa limejaa maji.


Amesema kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza uchunguzi na mnamo tarehe 18 Septemba, 2025 saa saba mchana huko maeneo ya njia panda ya viwandani, Kata ya Mlowo, Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa kuhusiana na tukio hilo.


Kamanda Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mtuhumiwa anadai alitekeleza mauaji hayo kwani mwaka 2023 alifika DDC Mbalizi akitokea Mbozi kwa ajili kufanya kazi kwa mama yake mkubwa aitwaye Judith Emmanuel ambaye ni mama mzazi wa marehemu kwa makubaliano ya kulipwa fedha kiasi cha shilingi laki moja (Tsh.100,000/=) kwa mwezi ambapo alifanya kazi kwa muda wa miezi mitano bila kulipwa ujira wake.


Ameeleza kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa mama huyo ambaye kwa wakati huo hakuwepo na kuanza kuiba vitu vya ndani kama sehemu ya kufidia fedha ambayo hakulipwa wakati ule ambapo akiwa anaendelea kufanya uhalifu huo, mtoto Rehema Sikalengo (arehemu) alimuona na kumwambia kuwa pindi mama yake atakaporudi atamueleza.


Anasema kutokana na kauli hiyo, ndipo mtuhumiwa aliamua kutekeleza mauaji hayo kwa lengo la kupoteza ushahidi.


Wakati huohuo jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya aliyekuwa Mwanachuo wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe ndaki ya Mbeya kitivo cha sheria aitwaye Shairose Michael Mabula (21) ambapo imeelezwa kuwa hapo awali mnamo tarehe 14 Septemba, 2025 Baba mzazi wa marehemu aitwaye Dkt Michael Mabula alifika katika kituo kikuu cha Polisi Mbeya na kutoa taarifa ya kupotea kwa binti yake aitwaye Shairose Mabula ambapo jalada la uchunguzi lilifunguliwa na kuanza ufuatiliaji ili kumpata.


Kamanda Benjamin Kuzaga wa Polisi Mbeya anasema mnamo tarehe 16 Septemba, 2025 saa 5 usiku huko katika Kata ya Isyesye Jijini Mbeya ilipokelewa taarifa ya ajali ya moto ambapo Askari walifika eneo la tukio na kukuta kibanda kinateketea kwa moto.


Amesema baada ya uchunguzi ilibainika kuna mwili wa mtu mmoja jinsia ya kike unaungua ambaye kwa wakati huo hakuweza kutambulika na mwili wa marehemu ulichukuliwa na kuhifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya na baada ya uchunguzi wa kitabibu na kuhusisha ndugu ilibainika kuwa mwili huo ni wa Shairose Mabula aliyekuwa anatafutwa baada ya kuripotiwa kupotea.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na uchunguzi wa kina ikiwemo uchunguzi wa kisayansi ili kubaini na kutambua mwili wa marehemu na kuwakamata waliohusika na mauaji ya binti huyo.


Pia jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa azitoe ili mkondo wa sheria kufuatwa ambapo pia Polisi mkoani Mbeya inaendelea kutoa rai kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo mauaji..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI