Header Ads Widget

MAONESHO YA SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2025 KUENDELEA KUFANYIKA GAIRO

 

Na Lilian Kasenene, Morogoro

KATIKA kuhakikisha wakulima mkoani Morogoro wanaondokana na kilimo chakula pekee,mkoa umejipanga kuendelea kuhamasisha kilimo biashara ili kuongeza uchumi kwa wakulima hao.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alibainisha  hayo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa rasmi ya maonesho hayo yanayojulikana kama “Samia Kilimo Biashara Expo 2025" yatakayofanyika wilayani Gairo kuanzia Septemba 28, mwaka huu.


Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro imeendelea na maonesho hayo ya kilimo ambayo hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kutoa elimu ya kilimo kwa wakulima na mara hii imejipanga kuhamasisha kilimo biashara.


RC Malima alisema Wilaya ya Gairo imekuwa ya mfano katika kutekeleza mapinduzi ya kilimo biashara kwa vitendo, jambo ambalo limeongeza mapato na kuwawezesha wakulima kunufaika moja kwa moja, kwa sababu hiyo, wilaya hiyo imechaguliwa kuendelea kuwa mwenyeji wa maonesho hayo.

"Katika haya mapinduzi ya kilimo, namba moja ni Gairo,” alisema Adam Malima.

Akifafanua zaidi, Mkuu wa Mkoa huyo alisema mkoa pamoja na Wilaya hiyo wamejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuwa kila zao linaweza kuwa zao la biashara endapo tu litazalishwa kwa wingi ama zaidi ya mahitaji ya chakula na hivo kuondokana na kilimo chakula.

Pia alisema Tanzania imeweka masukumo mkubwa kuelekea kuwa mzalishaji mkubwa Africa kupitia mapinduzi ya Kilimo yanayojikita katika Wilaya ya Gairo.

Alisema mpango wa Samia Kilimo Expo umeendelea kusukuma Kilimo Cha mazao ya kimkakati ikiwemo Karafuu,Parachichi na Mchikichi.


Aidha, Maonesho hayo yatakwenda kutoa Elimu ya kilimo biashara hususan matumizi ya  mbinu za kisasa za uzalishaji, matumizi ya teknolojia, usindikaji wa mazao, pamoja na kujenga mitandao ya kibiashara.


Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa Malima alisema, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kuhakikisha Mkoa wa Morogoro unakuwa kinara wa mapinduzi ya kilimo.


Hivyo, alitoa wito kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wote wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo ili wapate elimu ya mbinu bora za kilimo, teknolojia za kisasa na fursa za masoko zitakazoongeza tija na kipato chao.


Katika hatua nyingine,Malima alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, na kwamba uchaguzi siyo vita bali ni suala la kikatiba katika kuwapata viongozi watakaowaletea wananchi maendeleo yao na kuwataka wanahabari kutumia kalamu zao kuhamasisha uchaguzi huo kuwa wa AMANI, SALAMA na KISTAARABU.


Mkuu wa Wilaya ya Gairo Japhari Kubecha akizungumza katika mkutano huo alisema maonesho hayo ni kiini cha kuunganisha wadau katika mnyororo wa thamani na kuongeza uzalishaji wa mazao biashara.


Alisema maonesho yamesaidia wakulima kuelewa umuhimu wa Kilimo biashara na kuchangamkia fursa zaidi,na kueleza namna walivyojipanga maonesho hayo yanafikia kiwango Cha kimataifa


Maonesho ya 'SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2025' yatazinduliwa Septemba 28, 2025 na kufungwa Oktoba 4 mwaka huu.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI