Header Ads Widget

JE, RAILA ANA HOFU NA RUTO AMA ANAJIIMARISHA KISIASA?


Aliyekuwa waziri Mkuu nchini Kenya Raila Odinga

 ''Tulitia saini na kufanya makubaliano kwamba tutafanyakazi pamoja hadi 2027. Hatujapitisha makubaliano yoyote mbali na kupanga jinsi tutakavyoukabili uchaguzi ujao, kwa hivyo popote mulipo, musikishirikishe chama kwa mambo ambayo hayajazungumzwa.

Haya ndio yaliokuwa maneno ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wakati wa mkutano wa wabunge wa chama chake cha ODM mjini Machakos.

Raila alifafanua kuwa mpango wake wa kufanya kazi na Rais Ruto na utawala wa Kenya kwanza ulipaswa kukamilika 2027 na kwamba chama cha ODM hakitajifunga zaidi ya muda huo.

Matamshi ya Raila yanajiri huku kura ya maoni ya Tifa nchini Kenya ikisema kuwa idadi kubwa ya Wakenya ina amini kwamba Kiongozi wa ODM Raila Odinga atamuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027.

Waziri mkuu huyo wa zamani alisisitiza kuwa chama hicho hakijakosa mgombea 2027 na kwamba kitafanya maamuzi kulingana na michakato ya ndani na sheria.

Licha ya kwamba kiongozi huyo amekuwa akishirikiana na serikali ya rais Ruto katika kile kinachoitwa Broadbased Government {Serikali inayoshirikisha Wakenya wote} Raila aliwakumbusha wanachama wa chama hicho kwamba ODM haijapitisha makubaliano yoyote ya kumuunga mkono Rais Ruto kwa awamu ya pili.

''Sisi ni ODM. Nani alikuambia kuwa ODM haitakuwa na mgombea 2027? Tuna mpango wa wazi ambao tumejadiliana na kuafikiana.Tuendelee kutekeleza mpango huo. Maamuzi mengine yatachukuliwa wakati utakapofika'', Raila aliongezea.

Matamshi hayo yamezua mjadala mkubwa nchini Kenya na hata kuwatia tumbo joto wale waliokuwa wakijiandaa kumuunga mkono rais Ruto mwaka 2027.

Tayari kumekuwa na mvutano katika chama hicho ambapo baadhi ya viongozi wameonekana waziwazi wakiunga mkono azma ya Ruto kuchaguliwa tena kwa awamu ya pili na wengine wakishinikiza chama hicho kuandaa mgombea wake.

Wachanganuzi wanasema hali hiyo inasisitiza aina ya ushirikiano ambao Raila anapaswa kudumisha anapofanya kazi na Ruto kabla ya uchaguzi wa 2027.

Lakini Je, matamshi haya yalikuwa na maana gani kwa wafuasi wake, chama chake cha ODM na uchaguzi wa 2027?

Rais William Ruto na mshirika wake wa karibu Raila Odinga

KUJIFUA KISIASA.

Raila Odinga ameanza mikakati kadhaa ya kujiinua kisiasa baada ya miezi kadhaa ya kuonekana kushirikiana na Rais William Ruto hatua ambayo imezua mgawanyiko mkubwa katika chama chake cha ODM.

Kwa kudai kwamba Chama hicho huenda kikawa na mgombea wake , Raila Odinga anajaribu kuwaonesha tena wafuasi wake kwamba huenda akawa mgombea wa uchaguzi wa Urais wa 2027.

Raila anaamini kwamba ana nafasi nzuri ya kushinda Uchaguzi mwaka 2027 licha ya umri wake ambao umepigwa jeki na ushindi wa Peter Mutharika nchini Malawi ambaye ana umri wa miaka 85.

Lengo la kiongozi huyo ni kuhakikisha kwamba anachukua nafasi yake ya kisiasa nchini ambayo imekuwa ikitishiwa kuchukuliwa na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ambaye anadhibiti idadi kubwa ya kura za jamii kutoka Mlima Kenya iliompigia kura William Ruto 2022.

Vilevile anajiandaa kuwavutia tena wafuasi wake, ambao wengi wamekosa mwelekeo huku wengine wakijiandaa kumuunga mkono William Ruto.

Tayari chama chake cha ODM kimekuwa kikifanya mikutano ya mashinani kuadhimisha miaka 20 mbali na kuandaa chaguzi ili kujitayarisha kwa uchaguzi wa 2027.

KUIMARISHA UWEZO WAKE KATIKA MEZA YA KISIASA.

Baada ya kujifufua kisiasa na kuimarika, Raila Odinga atatumia uwezo wake na ule wa chama kukaa katika meza ya majadiliano na Rais William Ruto ili kuomba chochote anachotaka katika Muungano utakaounda serikali ijayo baada ya uchaguzi wa 2027.

Iwapo William Ruto atashindwa kumfurahisha Odinga kupitia nafasi za uongozi na zawadi kadha wa kadha, Raila atakuwa na chaguzi mbadala za kuwania Urais au kumuunga mkono mgombea wa upinzani hususan iwapo Kalonzo Musyoka atakabidhiwa bendera hiyo – kutokana na ukaribu wake na kiongozi huyo ambaye amewahi kumuunga mkono mara tatau katika azma yake ya kuwania urais.

Vilevile Raila ana ushirikiano wa karibu na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na kuna uwezekano mkubwa kwamba yeye{ Uhuru} anaweza kumshawishi Odinga kumuunga mkono mgombea anayepigiwa upatu na raia huyo wa zamani aliyekuwa waziri wa Elimu Fred Matiangi ambaye pia naye anatoka katika sehemu ya Nyanza ambayo ndio ngome kuu ya Raila Odinga.

Raila Odinga akiambatana na Rais William Ruto na naibu wa Rais kulia

KUZIMA HALI YA WASIWASI KATIKA CHAMA CHA ODM.

Kufuatia hatua ya Raila Odinga kushirikiana na serikali ya Rais William Ruto chama cha ODM kimekumbwa na misukosuko chungu nzima.

Baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakipinga ushirikiano wa chama hicho na serikali kama vile Katibu Mkuu wa chama hicho wamejipata katika hali mbaya wakishtumiwa kwa kwenda kinyume na matakwa ya kiongozi wa chama.

Vilevile kuna wale viongozi ambao wamevutiwa na Uongozi wa William Ruto na sasa wameanza kujiandaa kumsaidia rais huyo kuingia katika awamu ya pili.

Kwa kutoa tamko la kwamba Chama cha ODM hakijaingia katika makubaliano ya kumsaidia Ruto 2027, Raila Odinga alitaka wanachama wa chama cha ODM kuungana na kuwacha malumbano ambayo yamekuwa yakikizonga chama hicho na badala yake kuzungumza kwa sauti moja.

Anahisi kwamba ni kupitia umoja wa chama hicho pekee ambapo anaweza kukitumia kupigania maslahi yake .

JE, RAILA ODINGA ANA HOFU NA RUTO.

Raila na Ruto uwanjani Kasarani wakati wa mashindano ya CHAN

Katika siku za hivi karibuni Rais William Ruto amekuwa akishirikiana pakubwa na wandani wa Raila Odinga katika harakati zake za kuyavutia maeneo ambayo yalimpigia kura Raila Odinga kwa wingi katika uchaguzi mkuu uliopita.

Hatua hii inalenga kurudisha kura ambazo zinatoka eneo la Mlima Kenya ambalo kwa sasa linaonekana kumpa mgogo rais huyo kufuatia hatua yake ya kumtimua madarakani aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua anayetoka katika eneo hilo.

Viongozi kama vile Hassan Joho - waziri wa madini kutoka kwa Pwani ya Kenya ameonekana kwa karibu sana kushirikiana na rais William Ruto hatua ambayo imedaiwa kuzua hofu katika chama cha ODM.

Kulingana na mchangunuzi wa kisiasa David Burare baadhi ya viongozi katika chama hicho hawafurahishwi na hatua ya rais Ruto kushirikiana moja kwa moja na viongozi hawa badala ya Raila Odinga.

Hivyobasi wamemtaka Raila Odinga kujitokeza na kuchukua uongozi wa chama kisiasa ili kuhakikisha kwamba ushirikiano wowote kati ya Ruto na Viongozi huo unafanyika kupitia yeye.

''Ruto hangetaka kushirikiana na Raila Odinga ambaye ana nguvu au ushawishi mkubwa wa kisiasa hivyobasi analenga kupunguza ushawishi wake kupitia ushirikiano na viongozi waliopo mashinani na sio moja kwa moja na Raila', alisema bwana Burare.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI