Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imemhukumu Hemed Juma Mrisho maarufu kama Horohoro kwenda jela kutumikia kifungo cha maisha baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa gramu 326.46.
Hukumu hiyo ilisomwa Septemba 23, mwaka huu katika mahakama hiyo iliyoketi chini Jaji Sedekia Kisanya, baada ya kusikiliza mashahidi 14 na kupitia vielelezo 23 vilivyowasilishwa mahakamani na upande wa Jamhuri.
Ushahidi wa Jamhuri ulieleza kuwa, Horohoro alikamatwa Oktoba 31, 2023, Boko Magengeni,Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwa anaendesha gari aina ya BMW X5 lenye namba za usajili T189 DWY.
Ilidaiwa kuwa ndani ya gari hilo, maafisa wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA) walikamata mfuko wa rangi nyekundu wenye unga uliothibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kuwa ni cocaine yenye uzito wa gramu 326.46.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Gloria Kilawe akisaidiana na Marietha Maguta na Hamis Katandula, ulithibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na dawa hizo haramu.
Upande wa utetezi, ukiongozwa na Mawakili Augustine Kusalika na Nehemia Nkoko, ulipinga ushahidi kwa kudai kuwa mshtakiwa alikamatwa kabla ya tukio na kwamba kesi ilichochewa na chuki binafsi.
Hata hivyo, hoja hizo zilitupiliwa mbali na Mahakama, ikiridhia ushahidi wa Jamhuri.
Jaji Kisanya alisema ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umejitosheleza na kuthibitisha kosa bila kuacha shaka.
Aidha, Mahakama imetoa maagizo ya kisheria kuhusu vielelezo ikiwemo kuteketezwa kwa cocaine iliyokamatwa, kurudisha baadhi ya mali binafsi za mshtakiwa, huku gari lililotumika kusafirisha dawa hizo na fedha taslimu Sh. Milioni 4.1 zinataifishwa kwa hatua maalum za kisheria.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 (R.E. 2023), kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito unaozidi gramu 200 adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.Hivyo, hukumu hii ni onyo kali kwa jamii kwamba biashara ya dawa za kulevya haitavumiliwa nchini.
0 Comments