Header Ads Widget

DC, NGUBIAGAI AWATAKA VIJANA WALIOHITIMU MAFUNZO YA JESHI LA AKIBA UKEREWE KULILINDA TAIFA.

 

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, amewataka vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Akiba kushiriki katika ulinzi wa Taifa hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi, akisisitiza kuwa uwepo wa jeshi hilo ni kwa ajili ya kuimarisha amani na utulivu ndani ya jamii.

Hayo ameyabainisha jana wakati akifunga mafunzo ya askari 72 wa Jeshi la Akiba kutoka kata za Namilembe, Kakukuru na Ilangara, katika kijiji cha Nakamwa, kata ya Namilembe wilayani humo.


Ngubiagai aliwataka wahitimu hao kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri kwa kuonesha nidhamu na maadili kwenye jamii kwa lengo la kujenga mshikamano wa kitaifa.

“Ulinzi wa taifa letu ni jukumu la kila Mtanzania, na kila kijana anatakiwa kushiriki katika ulinzi, na sio mpaka msubirie nchi iwe katika machuko au mambo mbalimbali yanayoweza kusababisha nchi kuwa matatani ndio mshiriki katika ulinzi,” alisema Ngubiagai.


Kwa upande wake, Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Ukerewe, Nyamsha Dioniz, alisema mafunzo hayo yalianza Aprili 22, 2025 yakiwa na wanafunzi 58 na kumalizika na wahitimu 72.

Aliongeza kuwa wanajeshi hao wamejifunza masomo mbalimbali ikiwemo utimamu wa mwili, usomaji wa ramani, uhamiaji, kuzuia na kupambana na rushwa, ujanja porini, zimamoto, sheria za Jeshi la Akiba na mbinu za kivita ili wawe tayari kwa dharura za kitaifa na kuwaongoza wananchi kulinda amani.


Miongoni mwa wahitimu, Kamanda Paredi John Denis, akisoma risala, aliwataka vijana waliopo mitaani kujiunga na jeshi hilo ili kuondokana na fikra potofu kwamba kuingia mgambo ni kushindwa maisha, akibainisha kuwa tayari ana ujuzi anaoweza kutumia sehemu mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Ngubiagai aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni ya wagombea ili kusikiliza sera zao na ifikapo Oktoba 29, wamchague Rais, Mbunge na Diwani watakaowaletea maendeleo.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI