Na Moses Ng'wat, Songwe.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia fundi magari, Hussein Juma Halili (32), mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za kujaribu kuingiza nchini kiasi cha dola za Marekani 160,000 (zaidi ya Shilingi milioni 400) bila kuwa na maelezo ya uhalali wa fedha hizo.
Tukio hilo lilitokea Agosti 20, 2025 katika kituo jumuishi cha forodha (OSBP) Tunduma, ambako mtuhumiwa alikamatwa na askari polisi pamoja na maafisa wa vyombo vingine vya usalama akiwa katika harakati za kuvuka mpaka akitokea nchini Zambia.
Akizungumza na waandishi wa Habari Septemba 2, 2025, Kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, Austino Senga, alisema kuwa, baada ya upekuzi kufanyika, fedha hizo zilipatikana zikiwa zimehifadhiwa ndani ya koti alilokuwa amevaa mtuhumiwa.
"Mtuhumiwa baada ya kupekuliwa na askari polisi pamoja na maafisa wa vyombo vingine vya usalama alikutwa ameficha fedha hizo aina ya Dola za Marekani kwa kuzizungusha ndani ya koti lake huku akiwa amezibana na plasta" alifafanya Kamanda Senga.
Kamanda Senga alisema kuwa, mtuhumiwa huyo alikutwa na noti 1,525 kila moja ikiwa na thamani ya dola 100, pamoja na noti nyingine 150 ambapo kila moja thamani yake ni dola 50.
Aliongeza kuwa, mtuhumiwa anashikiliwa kwa mahojiano zaidi huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini chanzo na uhalali wa fedha hizo.
Aidha, Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu kama vile usafirishaji haramu wa fedha na bidhaa, na kuhimiza ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya dola katika kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha uhalifu mkoani humo.
0 Comments