Header Ads Widget

ZANA ZA KISASA ZABADILI MAISHA YA WAKULIMA – WAKULIMA WAASWA KUACHA MITAZAMO YA KIZAMANI


Wakulima mkoani Mbeya na maeneo ya Nyanda za Juu Kusini wametakiwa kuachana na kilimo cha mazoea na kuanza kutumia zana za kisasa ili kuongeza tija na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya kilimo.

Wito huo umetolewa na Mwita Peter Chacha, Afisa Masoko wa kampuni ya Agricom Africa LTD, alipokuwa akizungumza na kituo hiki  wakati wa kuhitimisha maonesho ya kilimo ya Nane Nane kwa mwaka huu, yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

"Tunawaomba wakulima waachane na zana duni walizozoea na kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa kama matrekta, vipandikizi, na mashine za kunyunyizia ili kuongeza uzalishaji. Kilimo cha sasa kinahitaji ubunifu na ufanisi,” amesema Chacha.

Mfano hai wa mabadiliko haya ni Frank Ambali, mkulima kutoka wilayani Mbarali, ambaye ameshuhudia mafanikio makubwa baada ya kubadili mtazamo wake na kuwekeza kwenye zana bora.

"Nikiwa bado natumia jembe la mkono, nilikuwa nalima hekari mbili au tatu tu kwa mwaka. Lakini sasa, natumia trekta na zana nyingine za kisasa, nalima zaidi ya hekari 50, na huvuna zaidi ya gunia 1,200 za mpunga kwa msimu," amesema Ambali kwa kujiamini.

Amesema teknolojia imemrahisishia kazi, imepunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija, huku akiwataka wakulima wengine kuacha hofu na mitazamo hasi dhidi ya zana za kisasa.

"Wapo wakulima wenzangu ambao bado wanadhani trekta ni kwa matajiri tu, au mashine ni kwa mashamba makubwa. Huo ni mtazamo wa kizamani. Kila mkulima anaweza kufanikisha kilimo bora kama atakuwa tayari kubadilika,” amesema Ambali.

Maonesho ya Nane Nane mwaka huu yameonesha msisitizo mkubwa kwenye matumizi ya teknolojia katika sekta ya kilimo, ikiwa ni pamoja na mashine, mbegu bora, na mifumo ya umwagiliaji, kama njia ya kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wakulima nchini. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI