Header Ads Widget

WMA, MWANZA WAPAMBANA NA UDANGANYIFU, WAKAMATA VIONGOZI WA VYAMA VYA MSINGI VYA PAMBA.


Na chausiku said Matukio Daima Mwanza.

Katika juhudi za kupambana na udanganyifu wa vipimo, Wakala wa Vipimo Mkoa Mwanza wamefanya ukaguzi wa kushitukiza na kuwakamata viongozi wa vyama vya pamba 30 kati ya vyama 46 vilivyobainika kuchezea mizani isiyo sahihi, hatua ambayo imeleta matumaini kwa wakulima waliokuwa wakiathirika.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa Mwanza, Hilarius Mnyavanu, alisema kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi walihusika katika uharibifu wa mizani kwa lengo la kuwapunja wakulima, jambo ambalo lilipigwa marufuku kwa nguvu na wakala.

“Katika operesheni yetu tulikuta mizani ilikuwa sahihi, lakini baadhi ya viongozi walitumia mbinu za kuharibu mizani ili kuwapunja wakulima,” alisema Mnyavanu..


Aliongeza kuwa hatua kali za kisheria zimechukuliwa dhidi ya viongozi hao, ikiwemo faini na marekebisho ya mizani ambayo sasa inatumika kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

Mnyavanu pia alisema kuwa lengo la Wakala wa Vipimo katika maonesho ya wakulima Nane Nane Jijini Mwanza ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo ili kuepukana na vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara.

“Tuko hapa kutoa elimu na kuwaelimisha juu ya taratibu za kushughulikia udanganyifu wa vipimo pale panapobainika,” alisema.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuwa makini wanapokuwa wanunuzi na kuripoti ofisi za Wakala wa Vipimo iwapo wataona udanganyifu wowote.


Kuhusu ufungashaji wa mizigo, Mnyavanu alisema Sheria inawataka wafanyabiashara kufunga mizigo isiyozidi kilo 100 ili kuepuka rumbesa katika usafirishaji.

Jeribrahimu, mkazi wa Nyasiha B Wilaya ya Magu, ambaye alitembelea banda la wakala wa vipimo, alisema amejifunza mambo mengi kuhusu haki za wateja na jinsi ya kushughulikia udanganyifu wa vipimo.

“Niliwahi kununuliwa bidhaa pungufu lakini sikuwa na maarifa ya kuripoti. Sasa nimepata uelewa na najua jinsi ya kujilinda,” alisema.

Wakala wa Vipimo unahakikisha kuwa matumizi sahihi ya vipimo yanaendelezwa kwa lengo la kulinda haki za watumiaji na wakulima katika Mkoa wa Mwanza


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI