WANAWAKE kupitia Baraza la Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Morogoro Mjini wameazimia kwa kauli moja kusahau tofauti zilizojitokeza wakati wa kura za maoni na kusimama pamoja kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Katibu wa UWT Morogoro Mjini, Bi Judith Joseph, aliwaambia wajumbe wa Baraza hilo kuwa huu sio wakati wa kugawanyika bali kushirikiana kikamilifu kuhakikisha Rais Samia Suluhu Hassan anapata ushindi mkubwa, sambamba na mgombea ubunge w Jimbo la Morogoro Mjini Abdulaziz Abood na madiwani katika kata zote 29 za manispaa.
“Ushindi tunaoutafuta ni wa chama chetu, si wa mtu binafsi. Wanawake tumekubaliana kuvunja makundi na kusimama bega kwa bega na Mama Samia,” alisema Bi Judith huku akishangiliwa na wajumbe.
Makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo mama lishe, wafanyabiashara wadogo, wauzaji wa bar na wanufaika wa mikopo ya halmashauri walihudhuria kikao hicho na kuahidi kushiriki kikamilifu kwenye kampeni kwa njia ya nyumba kwa nyumba ili CCM ipate ushindi wa kishindo.
Viongozi wa UWT akiwemo Leticia Ndomba na Redempta Mushi walibainisha kuwa mikopo ya wanawake iliyoanzishwa na Rais Samia imewasaidia akinamama wengi kujikwamua kwenye madeni ya mateso na sasa ni wakati wao kurudisha fadhila kwa kuhakikisha CCM inaibuka kidedea.
Aidha, wateuliwa wa viti maalum Immaculata Mhagama, Batuli Kifea na Latifa Ganzel walisisitiza kuwa watakuwa mstari wa mbele katika kusaka kura.
Wanawake hao pia walitoa wito kwa wananchi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara yake ya siku mbili Agosti 29 na 30, wakisema ujio wake utakuwa chachu ya mshikamano kuelekea ushindi wa CCM.
Mwisho.
0 Comments