Header Ads Widget

WANAOCHAKACHUA MBOLEA, MBEGU KUKIONA – RC MAKAME

 


Na Moses Ng'wat, Mbozi.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na uchakachuaji wa mbolea na mbegu za mahindi, akieleza kuwa vitendo hivyo si tu vinawaumiza wakulima bali pia vinahujumu uchumi wa taifa kwa ujumla.

Akizungumza Agosti 26, 2025, katika mji wa Vwawa, wilayani Mbozi, mara baada ya kufungua Kongamano la Wajasiriamali Wadogo lililofanyika katika viwanja vya stendi ya malori, RC Makame alisema serikali haitavumilia hujuma katika sekta ya kilimo.


"Kuna baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanachukua mbolea, wanaifungua na kuichakachua kisha kuijaza upya kwenye mifuko na kuiuza kwenye maduka ya pembejeo".

"Wengine huchagua mahindi mazuri kisha huyapaka rangi na kuyafunga kwenye mifuko yenye nembo za ubora na kuyauza kama mbegu kwenye maduka ya pembejeo," alisema Makame.

Alibainisha kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa chakula na kuvuruga maendeleo ya wakulima mmoja mmoja pamoja na uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.


“Tunaelekea kwenye msimu wa kilimo, serikali iko macho, haijalala na  tukikukamata utashitakiwa kwa sheria ya uhujumu uchumi na  siyo tena kwa sheria za kulipa faini za kawaida,” alionya vikali.

RC Makame aliagiza Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSC) na vyombo vingine vya serikali kuongeza kasi ya kufanya operesheni za mara kwa mara kwenye maduka ya pembejeo ili kuwabaini wanaokiuka sheria na kuwachukulia hatua kali.

Akielezea nafasi ya mkoa huo katika uzalishaji wa chakula nchini, Makame alisema mwaka uliopita Songwe ilizalisha tani milioni 1.6 za mahindi, huku mahitaji ya ndani yakiwa tani 360,000 pekee.


“Songwe ni miongoni mwa mikoa tegemeo kwa uzalishaji wa chakula nchini, tunapaswa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa ubora ili wakulima wazalishe kwa tija na kuchangia hifadhi ya chakula ya taifa,” alisema.

Aidha, Rc Makame alieleza kuwa serikali itaendelea kusimamia kwa karibu udhibiti wa mbolea ya ruzuku, ili kuzuia isitoroshwe kwenda nchi jirani, huku akisisitiza umuhimu wa mamlaka husika kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo bora, salama na zenye viwango vinavyotakiwa.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI