Header Ads Widget

WAKAZI WA MBABALA WATISHIA KUIHAMA CCM KWA KOTORIDHISHWA NA DIWANI MAYALA.

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media  Dodoma

BAADHI ya wakazi wa Kata ya Mbabala, jijini Dodoma, wametishia kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakieleza kutoridhishwa na hatua ya chama hicho kumpitisha tena aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Paskazia Mayala, katika kura za maoni, wakidai hajaleta maendeleoaaaaa yoyote katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake.

Wakizungumza jana katika ofisi ya CCM Wilaya ya Dodoma, wananchi hao walisema kuwa hawakumchagua Mayala katika kura za maoni, na wanashangazwa kuona jina lake likipitishwa, jambo linalowavunja moyo na kuwafanya kupoteza imani na chama chao.

 

Nyemo Selemona, mmoja wa wakazi wa Mbabala, alisema kuwa wapo tayari kumpigia kura mtu mwingine yeyote badala ya Mayala, hata kama ni jiwe, kwa madai kuwa hawajafaidika chochote katika kipindi chote cha uongozi wake.

 “Kiukweli sisi hatupo tayari kuongozwa na Mayala tena. Kwa miaka kumi alikuwa diwani lakini hakuna hata sekta moja aliyogusa kwa maendeleo. Tupo tayari kupigia kura jiwe kuliko kumchagua tena. Leo hatuondoki hapa ofisini mpaka kieleweke,” alisema Selemona kwa hasira.

Naye Juditha Mgaya, mkazi mwingine wa Mbabala, alisema kabla ya kufanyika kwa kura za maoni waliwasilisha malalamiko rasmi kwa chama kuhusu kutomtaka Mayala, lakini hawakusikilizwa, hali inayoonyesha wazi kupuuzwa kwa sauti ya wananchi.

“Tulipeleka malalamiko yetu kwa maandishi tukiomba Mayala asirudishwe kugombea, lakini chama hakuchukua hatua yoyote. Tunajiuliza kura zenyewe zilihesabiwa vipi hadi akapitishwa?” alisema Mgaya.

Wakazi hao walidai kuwa iwapo CCM haitazingatia maoni ya wanachama wake wa ngazi ya chini, ipo hatari ya chama kupoteza mvuto kwa wananchi, hususan katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao.


Kwa upande wake Pascazia Mayala alipoulizwa juu ya malalamiko ya wananchi kutokuwa na imani naye amesema kuwa yeye hawezi kuongea chochote kwani yeye ni mtoto wa CCM.

"Mimi siwezi kusema lolote kwani mimi ni mtoto wa Chama Cha Mapinduzi na chama ndo kilichonipitisha kugombea nafasi ya Udiwani hivyo wao wakamuulize aliyeniteua na nitaendelea kuongoza wao waache tu wapige kelele na nitawanyoosha"Ameeleza Mayala.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI