NA WILLIUM PAUL, SAME.
KAMPENI za kuwatambulisha Watiania wa Ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi zimehitimishwa jana ambapo katika jimbo la Same mashariki jumla wa Watia nia saba wameweza kutembea katika kata 14 na kukutana na Wajumbe wa Mkutano mkuu wa Jimbo.
Wagombea waliopitishwa kuwania ni Anna Kilango Malecel, Miryam Mjema, Andrea Chezue, Adam Mzee, Dkt. Peter Kibacha, Nickson Mjema na Daud Mambo.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha zoezi hilo, Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Same, Mohamed Ifanda alisema kuwa, zoezi la kuwatambulisha Watiania hao limemalizika kwa amani ambapo kila mgomba alipata nafasi ya kusema hoja zake na kuomba kura.
Ifanda alisema kuwa, chama kilitoa fursa kwa wagombea wote kunadi sera zake endapo atachaguliwa ataenda kufanya nini kwa wananchi ambapo katika jimbo la Same mashariki fursa hiyo imetumika kwa kila mgombea.
"Niwapongeze sana wagombea kwa kuonyesha nishamu na heshima pamoja na upole katika kuhakikisha mnanadi sera na kuomba kura kwa amani niwaombe endeleeni hivyo katika siku ya kesho ili wajumbe wapate fursa ya kuwachagua viongozi wanaowataka" Alisema Ifanda.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Same, Arafath Mbiruka aliwataka wajumbe wa Mkutano mkuu wa Jimbo la Same mashariki kutambua wagombea watakaowachagua watawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Mbiruka alisema kuwa, hivyo wanao jukumu la kuhakikisha viongozi wataowachagua wazingatie mustakabali wa Jimbo ili waweze kuwavusha.
"Jambo ambalo Wajumbe mnaenda kulifanya kesho mnapaswa kutambua kuwa halitajirudia tena mpaka baada ya miaka mitano hivyo jukumu la kuwachagua viongozi bora lipo katika mikono yetu hivyo msifanye makosa chagueni viongozi bara na sio bora viongozi" Alisema Mbiruka.
Aidha aliwataka wananchi na wanachama wa CCM ambao sio Wajumbe wa mkutano wa Jimbo kutojitokeza kesho katika eneo ambalo litakuwa limetengwa maalum kwa ajili ya mkutano mkuu huo kuchagua wagombea.
0 Comments