Marekani na Rwanda zimekubaliana kuwa nchi hiyo ya Afrika itapokea hadi wahamiaji 250 waliofukuzwa kutoka Marekani, msemaji wa serikali ya Rwanda na afisa mmoja aliliambia shirika la Reuters, huku utawala wa Rais Donald Trump ukichukua mkondo mkali juu ya wahamiaji.
Makubaliano yalioripotiwa kwa mara ya kwanza na Reuters, yalitiwa saini na maafisa wa Marekani na Rwanda mjini Kigali mwezi Juni, alisema afisa wa Rwanda, akitoa sharti la kutotajwa jina, na kuongeza kuwa Marekani tayari imetuma orodha ya awali ya watu 10 kuchunguzwa.
"Rwanda imekubaliana na Marekani kupokea hadi wahamiaji 250, kwa kiasi fulani kwa sababu karibu kila familia ya Rwanda imepitia magumu ya kuhama, na maadili yetu ya kijamii yamejengwa kuunganisha na kurekebisha," alisema msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo.
"Chini ya makubaliano hayo, Rwanda ina uwezo wa kuidhinisha kila mtu aliyependekezwa kwa ajili ya makazi mapya. Wale walioidhinishwa watapewa mafunzo ya wafanyakazi, huduma za afya, na msaada wa malazi ili kuanza maisha yao nchini Rwanda, na kuwapa fursa ya kuchangia moja ya uchumi unaokua kwa kasi zaidi duniani katika muongo mmoja uliopita."
Ikulu ya White House na Wizara ya Mambo ya Nje haikutoa maoni mara moja huku Idara ya Usalama wa Taifa ilielekeza maswali yaulizwe kwa Wizara ya Mambo ya Nje.
Rais Donald Trump analenga kuwafurusha mamilioni ya wahamiaji nchini Marekani na utawala wake umetafuta njia za kuwahamisha katika nchi zingine, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka wahalifu waliopatikana na hatia nchini Sudan Kusini na Eswatini.
0 Comments