Mhitimu kidato cha nne St Dominic Savio Iringa Robart Godfrey Mosha akivishwa mataji ya maua na Frolah Chang’a na mwenyekiti wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Mufindi Marcelina Mkini kulia ambae ni mjukuu wake
Na Matukio Daima Media, Mufindi
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Mufindi, Marcelina Mkini, amesema kuwa wanawake wa wilaya hiyo wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumpa kura za kishindo ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza Matukio Daima Media wakati wa mahafali ya kidato cha nne shule ya St Dominic Savio alipokuwa akimpongeza mjukuu wake Robart Godfrey Mosha kwa kuhitimu alisema kuwa kazi kubwa zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia ni za kihistoria na zimeacha alama kubwa kwa Watanzania, hasa wanawake ambao wamekuwa mstari wa mbele kufaidika na sera za maendeleo.
KAZI ZA KIHISTORIA ZA RAIS SAMIA
Mkini alieleza kuwa tangu Rais Samia alipoingia madarakani, miradi mingi ya maendeleo imeibuliwa na mingine kukamilishwa. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na uboreshaji wa huduma za afya kwa kujengwa vituo vya afya, zahanati na hospitali katika maeneo mbalimbali nchini.
“Leo hii mama mjamzito Mufindi hapati tabu kama zamani, anaweza kupata huduma ya upasuaji, vipimo na dawa karibu na eneo lake bila kulazimika kusafiri umbali mrefu. Hii ni heshima kubwa kwa wanawake, na ndio maana tunasema lazima tumshukuru kwa kura,” alisema Mkini huku akipigiwa makofi na wanachama.
Aidha, aliongeza kuwa sekta ya maji nayo imepata kipaumbele kikubwa chini ya utawala wa Rais Samia. Kwa sasa miradi ya maji safi na salama imewafikia wananchi wengi vijijini na mijini, hali ambayo imepunguza changamoto ya wanawake na watoto kusafiri umbali mrefu kutafuta maji.
“Kipindi cha nyuma tulikuwa tukibeba ndoo za maji kichwani kutoka mbali, lakini sasa Rais Samia ametutua ndoo kichwani. Tunapata maji karibu na makazi yetu na tunayo hakika ya ubora wake. Huu ni ushahidi wa dhahiri kuwa wanawake hawajawahi kupewa kipaumbele hivi kama kipindi hiki,” alisema Mkini.
JITIHADA ZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Akizungumzia suala la nishati safi ya kupikia, Mkini alisema serikali ya awamu ya sita imefanya jitihada kubwa kuhakikisha wanawake hawateseki tena kwa kutumia kuni na mkaa pekee, bali sasa wamewezeshwa kutumia gesi na teknolojia zingine rafiki kwa mazingira.
“Wanawake wengi vijijini walikuwa wakipata changamoto kubwa kukata kuni na kuathirika kiafya kutokana na moshi. Lakini sasa jitihada za Rais Samia zimewezesha hata wanawake wa vijijini kutumia nishati safi ya kupikia. Hii ni hatua kubwa ya kumkomboa mwanamke,” aliongeza.
MWANAMKE NA FURSA ZA ELIMU YA UFUNDI
Mkini pia alieleza namna Rais Samia alivyowekeza kwenye elimu ya ujuzi kupitia vyuo vya VETA, ili wanawake na wasichana wapate stadi za maisha zinazowawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Alisema kuwa kupitia mpango wa Mwanamke na Samia, akinamama wengi wamepata nafasi ya kusomea fani mbalimbali ikiwemo ushonaji, useremala, ufundi umeme, na upishi.
“Hii ni nafasi ya kipekee. Mwanamke sasa hawi tena shuhuda wa maendeleo, bali anashiriki moja kwa moja. Wanawake wa Mufindi wamepata ujuzi kupitia mafunzo haya na wanaweza kuanzisha biashara zao. Hii ndiyo maana tunaona ni lazima tushiriki kuhakikisha Rais wetu anapata ushindi wa kishindo,” alibainisha.
UWT KUWA CHACHU YA USHINDI
Mkini alisisitiza kuwa UWT Mufindi imeweka mikakati ya kuhamasisha wanawake kila kijiji na kila kata kuhakikisha wanaelewa thamani ya kazi zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita na hivyo kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
“Tutapita nyumba kwa nyumba, tutafanya mikutano ya hadhara na vikao vya vikundi vya wanawake ili kuhakikisha tunafikisha ujumbe. Lengo letu ni kuhakikisha kura za Rais Samia zinakuwa kura za kujaa na kumwagika hii ni ahsante yetu kwa kiongozi jasiri na mwenye maono makubwa,” alisema.
Aidha, alisema UWT haitabaki nyuma katika kuwahamasisha wanawake kuwachagua pia wagombea ubunge na udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa wote wanatekeleza kwa vitendo sera na ilani ya chama hicho.
“Tutapigania ushindi wa Rais, wabunge na madiwani wote wa CCM. Hatutakubali kuona juhudi hizi zikichezewa na wapinzani wanaokuja na maneno bila vitendo. Tunataka kuhakikisha tunaendeleza mafanikio haya,” alisema.
Kwa upande wao, baadhi ya wanawake waliohudhuria mkutano huo walieleza hisia zao kuhusu kazi za Rais Samia. Mama Edina Sanga alisema kuwa miradi ya maji imemsaidia kuokoa muda aliokuwa akitumia kutafuta maji na sasa anaweza kutumia muda huo kufanya shughuli za maendeleo ya familia.
“Hapo zamani nilikuwa nikipoteza saa tatu hadi nne kutafuta maji, lakini sasa bomba liko jirani kabisa. Namshukuru Rais Samia kwa kuona matatizo ya wanawake wa vijijini. Oktoba nitakuwa mstari wa mbele kumpigia kura,” alisema.
Naye Angela Kalinga , kijana wa kike aliyepata mafunzo VETA kupitia mpango wa Mwanamke na Samia, alisema: “Mimi nimejifunza udereva , na sasa ninaweza kuendesha gari hii ni ndoto iliyotimia kwa sababu bila mpango huu nisingeweza kusoma. Kwa kweli Samia ni mama wa maendeleo.”
0 Comments