Na Matukio Daima Media ,Morogoro.
UJENZI wa bwawa katika Shamba la Umwagiliaji Dakawa wilayani Mvomero, mkoani Morogoro unatarajiwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji na kuwasaidia wakulima kupata huduma ya uhakika kwa msimu wote, sambamba na hatua ya kujenga uzio kuzunguka mradi huo ili kulinda miundombinu na kupunguza uharibifu unaosababishwa na mifugo.
Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Juma Matanga, alisema hayo wakati akizungumzia Mipango ya Serikali kujenga bwawa bwawa kwaajili ya kuhifadhi maji wakati wa msimu wa mvua.
Akasema bwawa hilo litakaloanza kujengwa wakati wowote toka sasa litawezesha maji kupatikana wakati wote na hivyo kuongeza tija ya kilimo.
Aidha akasema Wana mpango pia kujenga uzio kuzunguka shamba la umwagiliaji DAKAWA na ujenzi wake utasaidia kudhibiti mifugo ambayo mara kwa mara ambayo imekuwa ikiingia katika mashamba na kuharibu miundombinu ya umwagiliaji pamoja na mazao ya wakulima.
Alisema ujenzi huo pia utapunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kutokana na mwingiliano wa shughuli za jamii hizo mbili.
"Uzio huu utasaidia kulinda miundombinu ya umwagiliaji, kuongeza tija ya kilimo na pia kupunguza migongano kati ya wakulima na wafugaji,” alisema Mhandisi Matanga.
Aidha, alibainisha baadhi ya changamoto zinazokabili mradi huo kuwa ni pamoja na mifugo kuvamia eneo la skimu na kusababisha uharibifu wa mazao, upotevu wa maji kutokana na ukosefu wa bwawa kubwa la kuhifadhi, pamoja na gharama kubwa za matengenezo ya miundombinu inayoharibiwa.
Hata hivyo, alisema Tume imeanza kuzitafutia suluhisho changamoto hizo kwa kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa bwawa jipya, kuimarisha ulinzi kupitia uzio na pia kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi wa wakulima na wafugaji ili kuondoa migongano ya mara kwa mara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Tume hiyo, Maria Itembe, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi kwenye skimu za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa chakula cha kutosha na cha ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.
“Tumeleta vijana wetu wapya hapa shambani ili wajifunze kazi kwa vitendo, waone namna gani wanavyoweza kusaidia wakulima na sio kubaki ofisini pekee. Rais Samia amewekeza fedha nyingi katika skimu hizi kwa lengo la kuleta matokeo chanya ya uhakika,” alisema.
Skimu ya Umwagiliaji Dakawa iliyoanzishwa mwaka 1982 kwa ushirikiano kati ya Serikali na Shirika la Chakula la Taifa (NAFCO), ina eneo la hekta 3,225.15 linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, huku hekta 2,000 zikimwagiliwa kwa sasa kupitia miundombinu iliyopo.
Wafanyakazi wapya 52 wa Kada 10 wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji walipata fursa ya kujionea shughuli zinazofanyika Katika eneo la mradi na changamoto zilizopo
Mwisho.
0 Comments