Header Ads Widget

TUME YA UCHAGUZI YAONDOA FOMU ZA UTEUZI WA WAGOMBEA URAIS BAADA YA MUDA WA PINGAMIZI KUKAMILIKA

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma

MKURUNGENZI wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),  Ramadhani Kailima, ameongoza watumishi wa Tume hiyo kuondoa fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizokuwa zimebandikwa kwenye ubao wa matangazo wa Tume, mara baada ya kupita saa 24 tangu kubandikwa kwake.

Fomu hizo zilibandikwa rasmi saa 10:00 jioni ya Agosti 27, 2025  siku ya uteuzi wa wagombea ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa masharti ya kisheria yanayohusu utoaji wa fursa ya kuweka pingamizi dhidi ya uteuzi wa mgombea wa Urais na Makamu wa Rais.

Kwa mujibu wa masharti hayo, pingamizi linaweza kuwasilishwa na mgombea mwingine wa nafasi ya Urais, Msajili wa Vyama vya Siasa, au Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya saa 24 tangu fomu hizo kubandikwa.



Zoezi la kuondoa fomu hizo limefanyika leo, Agosti 28, 2025 saa 10:00 jioni, likiwa ni hitimisho la muda wa kisheria uliotolewa kwa ajili ya kuweka pingamizi.


Hatua hiyo inaashiria kuendelea kwa mchakato wa uchaguzi mkuu kwa mujibu wa kalenda ya NEC, huku Tume ikisisitiza uwazi na ufuatiliaji wa karibu wa taratibu zote muhimu za uchaguzi.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI