DODOMA — Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (INEC) imekanusha madai yanayosambaa mitandaoni kwamba mfumo wake wa uchaguzi umeunganishwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na chama cha siasa.
Katika taarifa yake ya Jumamosi, INEC imesema madai hayo ni ya uongo na upotoshaji, ikisisitiza kuwa mfumo wa uchaguzi nchini unatumia njia za kawaida (manual) na hauna uhusiano wowote wa kielektroniki na taasisi za serikali au binafsi.
“Daftari la kudumu la wapiga kura halijaunganishwa na mfumo wowote. Utaratibu wa kupiga kura, kuhesabu na kutangaza matokeo unafanywa kwa njia ya kawaida,” alisema Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima.
Tume ilibainisha kuwa wapiga kura hutumia kadi ya kupigia kura pekee, siyo Kitambulisho cha Taifa, na majina yao husomwa hadharani kituoni kabla ya kuruhusiwa kupiga kura. Vyama vya siasa na mawakala wao pia walikabidhiwa daftari la wapiga kura baada ya uboreshaji.
INEC imewataka wananchi kupuuza taarifa hizo na kufuatilia chanzo rasmi cha tume, ikiwemo tovuti yake na kurasa za mitandao ya kijamii, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Soma zaidi taarifa hiyo kwa Umma:
0 Comments