Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
KATIKA hatua ya kuongeza thamani ya zao la korosho na kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetangaza kuanza usambazaji wa mashine 200 za kubangua korosho kwa mikoa inayolima zao hilo kwa wingi nchini.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Korosho uliofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuwa mashine hizo hazitagawiwa moja kwa moja kwa vikundi vya wakulima kama ilivyokuwa awali, bali zitasambazwa kupitia halmashauri ili kuhakikisha usimamizi madhubuti na matumizi endelevu.
“Mahitaji ya mashine za kubangua korosho ni makubwa sana katika mikoa yetu Kutoa mashine 50 haitoshi, ndiyo maana sasa tunaanza na 200 tukijua uhitaji halisi ni mkubwa zaidi,” amesema Waziri Bashe.
Ameeleza kuwa lengo la serikali ni kusitisha kabisa uuzaji wa korosho ghafi nje ya nchi kwa kuongeza usindikaji wa ndani, hatua itakayoongeza mapato kwa wakulima pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa.
“Zao la korosho linapaswa kuwa chanzo kikuu cha fedha za kigeni kwa sasa linaongoza mbele ya mazao mengine likifuatiwa na tumbaku tunataka kuongeza mchango wake kupitia usindikaji wa ndani,” amesisitiza.
Katika kuhakikisha uendelevu wa uzalishaji wa korosho, Waziri huyo pia ameelekeza wakuu wa mikoa kuanzisha vitalu vya miche ya korosho (nasari) ambavyo vitawashirikisha wanawake na vijana ili kuwawezesha kiuchumi kupitia uzalishaji wa miche hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ambaye alizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa wenzake, alisema mkoa wake umeanza rasmi kulima zao la korosho na una imani kuwa litafanya vizuri.
“Tunaahidi mkoa wa Singida tunakwenda kupindua meza kwa kuwa mkoa namba moja kuzalisha korosho kwa wingi,” amesema Dendego.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Francis Alfred, aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa bodi inaendelea kuimarisha masoko ya zao hilo kwa mwaka 2024/2025, sambamba na kuweka mikakati thabiti kwa msimu wa 2025/2026.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa mikoa na wilaya kutoka mikoa ya Singida, Ruvuma, Dodoma, na Mtwara, pamoja na viongozi kutoka Bodi ya Korosho, Chama cha Wadau wa Korosho Tanzania, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Athumani Kilundumya.
0 Comments