Header Ads Widget

TUKACHARU RAU FOREST KUWAGUSA WENYE MAHITAJI MAALUM

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA.

KILIMANJARO.Msitu wa Rau uliopo wilaya ya moshi  mkoani Kilimanjaro unaendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii na mazingira, huku idadi ya watalii na washiriki wa shughuli za uhifadhi ikiongezeka kwa kasi  kila mwaka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa  Tamasha la Tukacharu Rau Festival msimu wa tatu, Mhifadhi wa msitu huo, Bw. Ullomi, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tukacharu Rau Forest mwaka 2023, mafanikio yamekuwa makubwa kutokana na watalii kuendelea kutembelea msitu huo.

Ameeleza kuwa katika msimu wa kwanza, wa Tukacharu Rau Festival walipokea watalii 6,500, na msimu wa pili idadi hiyo ilipanda hadi 11,800 na kusema  Kwa msimu huu wa tatu, wanatarajia kufikia hadi watalii 20,000, ikiwa ni ongezeko kubwa linalovunja rekodi za awali.


amesema kuwa msimu wa kwanza walikuwa na washiriki 360, na msimu wa pili walifikia 670 na kusema Matarajio kwa msimu huu ni kuvuka kiwango hicho.

Awali akizindua Tamasha hilo mkuu wa wilaya ya moshi Godfrey Mzava amesema  serikali inaendelea kuunga mkono jitihada za kuimarisha utalii wa ndani, ambao una nafasi kubwa ya kuchangia uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi.

Ameendelea kusema kuwa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa mdau namba moja katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya sekta ya utalii nchini na  juhudi zake hizo zimechangia ongezeko la watalii na mapato katika sekta ya utalii.

Mratibu wa tukio hilo, Rosemary Didas, alisema lengo kuu la Tukacharu ni kurudisha kwa jamii ikiwa ni pamoja ma kuwapa fursa wahitaji kutembelea msitu huo kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya Msitu huo.

"Tutawasaidia mahitaji yao muhimu kama vile vyakula ,vifaa tiba ,vifaa vya shule kwa wale watoto na mahitaji mengine "alisema Rosemary .

Wasimamizi wa vituo vya kulelea watoto wenye uhitaji  wamesema kuna changamoto wanayopitia watoto wenye uhitaji hivyo jambo hilo lililofanywa na uongozi wa msitu wa rau lina umuhimu sana kwani inawapa wenye uhitaji nafasi ya kutembelea msitu huo na pia kuwapa fursa ya kukutana na watu mbalimbali.

Tukacharu Festival  imelenga kuhamasisha utalii wa mazingira, uhifadhi wa vyanzo vya maji, na kuongeza uelewa wa mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kitaifa kulinda rasilimali asilia.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI