Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Upatikanaji wa huduma za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) visiwani Zanzibar umefungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Kupitia mikopo nafuu, elimu ya kifedha na uhusiano wa moja kwa moja na masoko ya uhakika, TADB imeibuka kama mkombozi wa kweli kwa wananchi wanaojihusisha na uzalishaji wa chakula na shughuli nyingine za kilimo ikiwemo mifugo na uvuvi.
Meneja wa TADB Zanzibar, Ally Jamal Singoi alisema jana kuwa benki hiyo imewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji, ufugaji wa kisasa, uvuvi endelevu, usindikaji wa mazao ya kilimo.
Alisema TADB imewezesha biashara ndogondogo zinazoendeshwa na vijana na wanawake kwenye minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Alisema jitihada hizi za TADB zimeleta matokeo chanya ikiwemo kuongeza tija, ajira, kipato na upatikanaji wa chakula katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema kupitia ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mashirika ya umma na yasiyo ya kiserikali, vyama vya ushirika, vikundi vya wanawake na vijana pamoja na mashamba ya pamoja, wananchi wengi waliokuwa hawajapata huduma za kifedha sasa wamewezeshwa kuwekeza katika mbinu bora za uzalishaji.
Alsiema wananchi hao wamefanikiwa kupata pembejeo bora, vifaa vya umwagiliaji, teknolojia za kisasa, na kupata masoko ya uhakika kwa mazao yao.
“Hadi sasa jumla ya miradi 43 imenufaika moja kwa moja na huduma hizi, ikiwemo miradi 7 inayomilikiwa na wanawake na miradi 4 ikiwa ni vijana . Sanjari na hayo jumla ya miradi10 imefadhiliwa ikiwa inamilikiwa na vyama vya ushirika (8 kutoka Pemba na 2 kutoka Unguja). Miradi yote hii imeunganishwa katika mifumo rasmi ya kibenki na masoko,” alisema.
Alisema TADB kupitia Kanda yake ya Zanzibar imewezesha miradi inayohusisha uzalishaji wa mazao ya biashara kama karafuu, ufugaji wa kuku wa mayai, uvuvi wa samaki kwa vizimba, pamoja na kilimo mseto kinachowahusisha vijana na wanawake.
Aidha, alisema benki imekuwa ikitoa mafunzo ya kilimo biashara na ujasiriamali kwa wakulima wapya jambo lililowasaidia kubadili mtazamo kutoka kilimo cha kujikimu hadi kilimo chenye tija na faida.
Alisema kupitia mradi wa Tanzania Inclusive Producers and Processors Partnership in Dairy (TI3P), TADB imeunganisha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa na wasindikaji katika mnyororo wa thamani wa maziwa.
Alisema mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na: Heifer International Tanzania, CARE Tanzania, IDH – The Sustainable Trade Initiative, Zanzibar Dairy Development Authority (ZDDA) na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo ya Zanzibar.

Alisema TI3P imelenga kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuboresha miundombinu ya ukusanyaji, kuhakikisha ubora wa bidhaa na kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika tasnia ya maziwa.
“Mpaka sasa zaidi ya wanufaika 200 wameshafikiwa kupitia mradi huo ambapo jumla ya ng’ombe wa maziwa (Improved heifers) 352 wenye thamani ya shilingi 993,294,050 zimetolewa vilevile wafugaji hao waliopatiwa mikopo wamepewa ruzuku fungamanifu zenye thamani ya TZS 222,000,000 ili kuwapunguzia mzigo wa ulipaji mikopo ili kuongeza tija na uzalishaji,” alisema.
Alisema kwa kushirikiana na Idara ya Mifugo Zanzibar na Shirika la Heifer International Mradi huu pia umewezesha elimu ya ufugaji bora, uhimilishaji wa kisasa, upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, lishe bora, na uwezeshaji wa vifaa kama pikipiki za maafisa ugani, mashine za kukatia majani, vifaa vya tiba, kompyuta na miundombinu ya ukusanyaji maziwa, jumla ya wafugaji 1583 (wanawake 453) wamefikiwa.
Alisema TADB inaendelea kuweka nguvu katika uwekezaji wenye mwelekeo wa mabadiliko ya kudumu kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali.
0 Comments