Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima, Dodoma
MCHAKATO wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuwapata wagombea wa ubunge katika majimbo ya Dodoma Mjini na Mtumba umefanyika kwa mafanikio, ambapo Samwel Malecela na Anthony Mavunde wameibuka washindi katika majimbo hayo husika.
Matokeo hayo yalitangazwa rasmi na Msimamizi wa uchaguzi wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Irimina Nyakato Mushonge, aliyebainisha kuwa zoezi la upigaji kura lilifanyika Agosti 4 na kukamilika usiku, jambo lililosababisha matokeo kutangazwa Agosti 5 jioni.
Katika Jimbo la Dodoma Mjini, jumla ya wajumbe walioshiriki walikuwa 9,502 ambapo kura zilizopigwa ni 6,288, zilizoharibika 82 na kura halali zilizohesabiwa zilikuwa 6,226. Samwel Malecela alipata kura 2,804 sawa na asilimia 43 ya kura halali, akitangazwa mshindi dhidi ya wagombea wengine saba.
Wagombea waliomfuatia ni Samwel Kisaro aliyepata kura 1,541 sawa na asilimia 23, Paschal Kinyele kura 641 (asilimia 10), Robert Mwinje kura 460 (asilimia 7.1), Abdulhabib Mwanyemba kura 459 (asilimia 7.19), Rosemary Jairo kura 132 (asilimia 2.1), Mhandisi Rashid Mashaka kura 118 (asilimia 1.8), na Fatuma Yusuph Waziri kura 52 sawa na asilimia 0.8.
Kwa upande wa Jimbo la Mtumba, jumla ya wajumbe walikuwa 11,555. Kura zilizopigwa zilikuwa 7,446, kati ya hizo 94 ziliharibika na 7,352 zilikuwa halali. Anthony Mavunde alipata kura 6,082 sawa na asilimia 80.9, akifuatiwa na Mussa Luhamo aliyepata kura 906 sawa na asilimia 12, Anthony Kanyama kura 274 (asilimia 3.6), na Mwajuma Karabaki kura 90 sawa na asilimia 1.2.
Licha ya uchaguzi huo kuendeshwa kwa amani na utulivu, baadhi ya wagombea wa Jimbo la Dodoma Mjini walikataa kusaini makubaliano ya matokeo wakieleza kuwepo kwa malalamiko ambayo kwa mujibu wa maelezo ya msimamizi wa uchaguzi, hayatafanyiwa kazi hadi yawasilishwe kwa maandishi katika ofisi za chama.
Matokeo hayo yanatarajiwa kupelekwa katika ngazi za juu za chama kwa ajili ya uteuzi rasmi wa wagombea watakaobeba bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
0 Comments