Na,Jusline Marco:Arusha
Umoja wa Wanakijiji waishio katika kingo za Ziwa Natron, wilayani Ngorongoro, wametoa tamko la jumla kupinga hatua za kampuni iitwayo Ngaresero Valley, kutaka kujenga kiwanga kitakachokuwa kinavuta maji kwa wingi kutoka ziwani kwa ajili ya kuchakata Magadi.
Muungano wa vijiji tisa vilivyopo katika kata za Engaresero na Magadini kwenye wilaya za Ngorongoro na Longido, Mkoani Arusha ukiongozwa na mwenyekiti wa umoja huo, Joshua Muriatoi Mollel, wamesema kuwa hatua ya mwekezaji huyo ni kinyume cha maagizo ya serikali ya Tanzania kwamba miradi kama hiyo isitekelezwa karibu na ziwa.
“Serikali imekwisha tenga eneo la kuchimba Magadi soda ambalo liko Engaruka, wilayani Monduli na tayari wananchi wa kule wamelipwa fidia ya mabilioni kwa ajili ya kuyaachia maeneo husika,” alisema Mollel.
Serikali, kupitia kampuni ya Maendeleo ya Taifa (NDC) ilitenga zaidi ya kilometa za mraba 245 katika eneo la Engaruka kwa ajili ya miradi ya uwekezaji kwa uvunaji wa madini ya Magadi Soda.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Engaresero, Khalid Abdallah Rashid, amekiri kuwepo mpango wa kujenga kiwanda cha Magadi katika wigo wa ziwa Natron, hata hivyo amesema bado hawajapewa kibali kwa ajili ya mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo amesema kuwa ingawa hivi karibuni kumefanyika tafiti kadhaa katika ziwa Natron, lakini suala la kuwekeza kiwanda cha Magadi katika mwambao wake, halipo kabisa.
Naye Mzee wa kimila wa kijiji cha Wosiwosi, Daniel Lemomoi, alisema mwekezaji huyo anasema anahitaji zaidi ya hekta 45,000 kwa ajili ya mradi huo, ikiwemo maeneo ya kulaza mabomba, pampu kubwa na kiwanda kikubwa cha kuchakata Magadi soda.
“Hatuna ardhi kubwa kiasi hicho, labda wanataka kutuhamisha wanakijiji, huu ni mradi wa kuangamiza maisha yetu na urithi wa taifa,” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Engaresero, James Sapuro Lywangiri, alisema serikali ilishawahi kuelekeza kuwa miradi ya aina hiyo iendelee kutekelezwa maeneo ya mbali zaidi, ikiwemo Kata ya Engaruka wilayani Monduli, na si kandokando ya Ziwa Natron.
Katika hatua nyingine Emmanuel Mgimwa, Mratibu wa Afrika Mashariki na Kusini wa IUCN-SSC Flamingo Specialist Group, alisema uchimbaji wa Magadi soda utahitaji kufyonza maji mengi kutoka ziwani na hata kubadilisha mtiririko wa mito muhimu, ikiwemo Mto Ewaso Ng’iro kutoka Kenya, jambo litakalosababisha kuvurugika kwa usawa wa maji na kuhatarisha kabisa uzalishaji wa flamingo.
Wataalamu wa mazingira wameonya kuwa Ziwa Natron ni mfumo dhaifu wenye usawa wa alkali, kifizikia na kikemikali, unaoweza kuharibika haraka kutokana na shughuli za binadamu ambapo Ziwa Natron limepewa hadhi ya kimataifa kupitia Mkataba wa Ramsar, likiwa kimbilio la ndege zaidi ya 100,000 wa maji na samaki adimu Oreochromis alcalicus, pamoja na mwani wa Spirulina platensis unaolisha flamingo.
Kwa upande wao wanaharakati wamesisitiza kuwa kulinda ziwa hilo ni jukumu la kikanda na kimataifa kwa kuwa ndege aina ya flamingo wanaozaliana humo husambaa katika maziwa ya Kenya, Uganda na Tanzania.
Wakati huo huo, Serikali kupitia NDC tayari inaendeleza mradi wa soda ash katika eneo la Engaruka wilayani Monduli, unaotarajiwa kuzalisha nusu milioni ya tani kwa mwaka kwa ajili ya mradi huo, ambapo zaidi ya kaya 595 zimelipwa fidia ya takribani shilingi bilioni 14.5 kupisha utekelezaji wake.
0 Comments