Na Moses Ng'wat, Mbozi.
Tume huru ya Taifa ya uchaguzi nchini Tanzania (INEC)
Imefanya uteuzi wa wagombea saba wa ubunge katika majimbo mawili ya Mbozi na Vwawa Wilayani Mbozi, kati ya wagombea tisa waliochukua fomu za kuomba uteuzi.
Katika uteuzi huo mgombea wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) jimbo la Mbozi, Michael Mwamlima, aliyechukua fomu za uteuzi aliingia mitini kwa kushindwa kuzirejesha INEC, huku mgombea wa chama
Chama cha Maarifa, Kilimo na Nishati (MAKINI), jimbo la Vwawa,
Onesmo Kapungu, akienguliwa katika kinyanganyori hicho baada ya kukosa sifa.
Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo hayo, Dani Tweve, alieleza kuwa mgombea wa chama cha MAKINI, Kapungu, ambaye aligombea ubunge katika jimbo la Vwawa kupitia chama cha hicho alienguliwa baada ya kubainika kuwa wadhamini wake wote si wakazi wa jimbo hilo.
Tweve alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi namba 1 ya mwaka 2024, kifungu cha 23(3)(d), hali hiyo ndiyo iliyosababisha mgombea huyo kukosa sifa na kuenguliwa.
Aidha, Tweve alisema mgombea wa chama cha CHAUMA katika jimbo la Mbozi licha ya kuchukuwa fomu ya kuomba kuteuliwa hakuweza kurejesha fomu na hivyo kukosa nafasi ya kuingia kwenye mchakato wa uteuzi.
Hata hivyo, aliwataja walioteuliwa katika jimbo la Vwawa kuwa ni Japhet Ngailonga Hasunga (CCM),
Enock Sikafunje Mwalukasa (CUF), Peter Asajile Kayuni (ACT-Wazalendo) na Happnes David Kwilabya (Chauma).
Kwa upande wa Jimbo la Mbozi, walioteuliwa ni Onesmo Mkondya (CCM),
Elia Ezekia Zambi (ACT-Wazalendo) na
Nkunyuntila Barton Siwale (CUF).
0 Comments