Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaosaidia Kuleta Utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) umelaani vikali mashambulizi yaliyofanywa na kikundi cha waasi wa Allies Democratic (ADF) kati ya 9 na 16 Agosti 2025, katika maeneo kadhaa ya Beni na Lubero, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
MONUSCO imesema mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu takriban 52 na huenda idadi hiyo ikaongezeka.
MONUSCO imeongeza kuwa vurugu hizo ziliambatana na matukio ya utekaji nyara, uporaji, uchomaji wa majumba na magari na uharibifu wa mali za raia ambao tayari wanakabiliana na mgogoro wa kibidamanu.
“Mashambulizi hayo yaliyolenga raia ambayo ni pamoja na mauaji yaliyotekelezwa usiku wa tarehe 26 hadi 27 Julai huko Komanda eneo la Irumu, Ituri, hayakubaliki na ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu,’’ taarifa ya MONUSCO ilisema.
Ujumbe huo umetoa wito kwa serikali ya DR Congo kufanya uchunguzi wa kina na kuwajibisha waliohusika na mauaji ya raia.
MONUSCO imetoa hakikisho la kuendelea kuunga mkono serikali ya Congo na jamii za wenyeji kuzuia ghasia zaidi, kulinda raia pamoja na kuchangia urejeshaji wa utulivu katika maeneo yalioathirika na vita.
0 Comments