Header Ads Widget

MWAJUMA MIRAMBO AANIKA VIPAUMBELE VYA UMD: UHURU, AFYA, ELIMU NA MIUNDOMBINU

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma


MGOMBEA urais wa Chama cha  Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Mirambo,ameaahidi kama atakuwa Rais atahakikisha watanzania wanapata haki zao huku akileta mageuzi makubwa katika sekta za afya, elimu na miundombinu. 

Akizungumza leo Agosti 11,2025 jijini Dodoma mara baada ya kukabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele jijini Dodoma, Mirambo akiwa na mgombea mwenza,Mashavu Alawi Haji amewasihi Watanzania kutoa nafasi kwa viongozi wapya wenye maono ya kweli ya maendeleo jumuishi, akisisitiza kuwa UMD ni chama kinachoamini katika kuwapa watu mamlaka na sauti. 


“Tunaamini katika uhuru wa Mtanzania kufanya kazi zake bila kikwazo; lakini uhuru huo lazima uambatane na haki, usawa na ulinzi wa maslahi ya wote,” alisema Mirambo mbele ya umati wa wafuasi wake.

Afya ya Mama na Mtoto Kipaumbele cha Taifa

Katika sekta ya afya, mgombea huyo alieleza dhamira ya serikali yake kuweka mkazo maalum kwenye afya ya mama na mtoto amesema hali ya huduma wakati wa ujauzito na kujifungua bado ni changamoto kubwa kwa familia nyingi, hasa vijijini.


“Watanzania hawawezi kuwa na afya bora bila kuwa na uchumi bora. Serikali yetu itawekeza kwenye vituo vya afya, vifaa tiba, na motisha kwa wahudumu wa afya kote nchini,” amesisitiza.

Elimu Bora 

Elimu ikiwa ni miongoni mwa nguzo kuu,  Mirambo aliahidi mageuzi ya mfumo wa elimu kwa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora, bila ubaguzi, na inayozingatia ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira.

Amesisitiza kuwa serikali ya UMD itawekeza katika mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuboresha maslahi ya walimu.


Miundombinu Imara kwa Uchumi Endelevu

Akizungumzia sekta ya miundombinu, Mirambo ameeleza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kufikiwa bila uwekezaji madhubuti katika barabara, maji safi, umeme wa uhakika, na miundombinu ya mawasiliano vijijini.

 “Tunahitaji miundombinu ya kisasa itakayofungua fursa za uchumi na biashara kila kona ya nchi hatutaki maendeleo ya mijini pekee, bali kwa kila Mtanzania, kila mahali,” ameongeza.


Sera za Majimbo na Ukusanyaji wa Kodi Rafiki

Katika kulinda usawa wa maendeleo nchini, UMD inakuja na sera za majimbo zinazolenga kugatua madaraka hadi ngazi ya chini, ili wananchi washiriki kikamilifu katika kupanga na kusimamia maendeleo ya maeneo yao.


Ameongeza kuwa serikali ya UMD itahakikisha kodi zinakusanywa kwa njia rafiki na yenye ufanisi, huku kipaumbele kikiwa ni kuhakikisha fedha hizo zinarudi kwa wananchi kupitia huduma bora.

 “Watanzania wamechoshwa kulipa kodi bila kuona matokeo yake tunataka kodi itumike kuwahudumia watu, si kuwabebesha mzigo wa matumizi yasiyoeleweka,”amesema Mirambo.

Mpaka sasa waliochukua fomu ni wagombea  8 ambao ni Samia Suluhu Hassan (CCM),Coaster Kibonde (Chama Makini),Doyo Hassan Doyo (NLD),Kunje Ngombare Mwiru (AAFP) Hassan Almas (NRA) na Twalib Kadege (UPDP) Georges Bussungu (ADA TADEA) 


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI