Header Ads Widget

TLP YAAHIDI ELIMU NA MATIBABU BURE KWA WATANZANIA

 

Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma

MGOMBEA wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira, leo amechukua rasmi fomu ya kugombea urais katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma, akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake Amana Suleiman Mzee.

Akionge na vyombo vya habari leo Agosti 11,2025 mara baada ya kuchukua fomu, Rwamugira ametangaza kuwa moja ya vipaumbele vyao vikuu ikiwa watapewa ridhaa ya kuongoza taifa ni elimu bure na matibabu bure kwa kila Mtanzania.


 “Sisi tunasema elimu bure, matibabu bure hatuwezi kuwa na taifa lenye uchumi imara bila  kuwa na wananchi wenye afya bora na elimu sahihi kuanzia chekechea hadi chuo kikuu,” amesisitiza Rwamugira mbele ya waandishi wa habari na wafuasi wa TLP.

Ameeleza kuwa TLP itawekeza kwenye elimu ya ufundi kuanzia ngazi za chini kabisa za elimu ili kuwaandaa vijana kuwa na ujuzi wa moja kwa moja wa ajira. 

Aidha, amesema kuwa huduma za afya zitaboreshwa kwa kuhakikisha hospitali zote nchini zinakuwa na dawa, vifaa, na watumishi wa kutosha.

 “Leo hii mtu anaumwa hana hela ya dawa, anafariki na familia inadaiwa hadi gharama za kuzikwa hali hii haikubaliki. TLP tutasimamia sera ya matibabu bure na mifuko ya bima kwa kila Mtanzania  hata bodaboda, mfugaji na mzoa taka lazima awe na bima ya afya,” alisema kwa msisitizo.
Chama hicho kimeahidi pia kuwa ndani ya miaka mitano, kitasimamia ipasavyo rasilimali za nchi ili ziwanufaishe wananchi wote na kusaidia kutoa ajira kwa vijana walio wengi walioko mitaani bila kazi.

Yustas Rwamugira anakuwa mgombea wa tisa kuchukua fomu ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Octoba mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI