Header Ads Widget

ISRAEL YAUA MWANAHABARI MASHUHURI WA AL JAZEERA NA WENZAKE 4 KATIKA SHAMBULIO LILILOELEKEZWA GAZA

 

Kituo cha habari cha Al Jazeera kimethibitisha kwamba waandishi wake watano wameuawa katika shambulio la anga la Israel lililotokea karibu na lango kuu la Hospitali ya Al-Shifa, mjini Gaza.

Miongoni mwa waliouawa ni mwandishi mashuhuri Anas al-Sharif, ambaye Israel imemtuhumu kuwa mwanachama wa Hamas.

Kwa mujibu wa taarifa ya kituo hicho, waandishi wa habari Anas al-Sharif na Mohammed Qreiqeh, pamoja na wapiga picha Ibrahim Zaher, Mohammed Noufal na Moamen Aliwa, walikuwa ndani ya hema maalum la waandishi wa habari lililokuwa limewekwa katika hospitali hiyo, wakati walipolengwa moja kwa moja na shambulio hilo la Jumapili.

Al Jazeera imelitaja tukio hilo kama “mashambuli mengine ya wazi na ya kupangwa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.”

Hata hivyo Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilithibitisha baadaye kuwa lilimlenga Anas al-Sharif, likidai kupitia chapisho la Telegram kwamba alikuwa kiongozi wa kikosi cha wapiganaji wa Hamas.

IDF haikuwataja wala kueleza lolote kuhusu waandishi wengine waliouawa.


Jumla ya watu saba waliuawa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa ripoti ya Al Jazeera

Kituo hicho awali kilitangaza kuwa wafanyakazi wake wanne wamepoteza maisha, lakini baadaye kilisasisha idadi hiyo na kuthibitisha kuwa ni watano.

Mhariri mkuu wa Al Jazeera, Mohamed Moawad, aliiambia BBC kuwa Anas al-Sharif alikuwa mwandishi aliyeidhinishwa rasmi, na ndiye aliyekuwa “sauti pekee inayoeleza ulimwengu kinachoendelea ndani ya Ukanda wa Gaza.”

Kwa kuwa waandishi wa kimataifa hawajaruhusiwa na Israel kuingia Gaza kuripoti kwa uhuru tangu kuanza kwa vita, vyombo vingi vya habari duniani vimekuwa vikiwategemea waandishi wa eneo hilo kupata taarifa kutoka ndani ya Gaza.

“Walilengwa wakiwa kwenye hema lao, hawakuwa mstari wa mbele wa mapigano,” alisema Moawad.

“Ni wazi kuwa serikali ya Israel inalenga kunyamazisha sauti yoyote inayoripoti kutoka ndani ya Gaza,” aliongeza katika mahojiano na kipindi cha The Newsroom.

“Hili ni jambo ambalo sijawahi kulishuhudia katika historia ya kisasa ya uandishi wa habari,” alisisitiza.

Anas al-Sharif, mwenye umri wa miaka 28, alionekana kuchapisha ujumbe kwenye mtandao wa X dakika chache kabla ya kuuawa, akiandika kuhusu mashambulizi makali ya mabomu yaliyoendelea mjini Gaza.

Chapisho lililofuata, ambalo linaaminika kuwa liliandaliwa mapema, lilichapishwa na rafiki yake baada ya taarifa za kifo chake.

Katika video mbili za kusikitisha zilizosambaa mitandaoni na kuthibitishwa na idara ya uhakiki ya BBC (BBC Verify), wanaume walionekana wakibeba miili ya waliouawa.

Wengine walionekana wakilitaja jina la Qreiqeh kwa uchungu, huku mtu mmoja aliyevalia fulana iliyona chapa ya “vyombo vya habari” akisema kuwa mmoja wa marehemu ni Anas al-Sharif.

Katika taarifa yake, IDF ilimshutumu al-Sharif kwa kujifanya mwandishi wa habari, ikidai kuwa alikuwa “mhusika mkuu katika kupanga mashambulizi ya roketi dhidi ya raia wa Israel na wanajeshi wa IDF.”

Jeshi hilo lilidai kuwa tayari lilikuwa limesambaza taarifa za kijasusi zinazoonesha ushiriki wa al-Sharif katika mafunzo ya kijeshi.

Mwezi mmoja kabla ya kuuawa kwake, Mtandao wa Al Jazeera, Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (CPJ) walitoa taarifa tofauti wakionya kuwa maisha ya al-Sharif yalikuwa hatarini na kutoa wito wa kulindwa kwake.

Mkurugenzi Mtendaji wa CPJ, Bi Jodie Ginsberg, aliliambia BBC kuwa mamlaka za Israel zimeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha madai yao kuwa waandishi waliouawa walikuwa magaidi.

“Huu ni mwenendo ambao tumeushuhudia kutoka Israel si katika vita vya sasa pekee, bali kwa miongo kadhaa iliyopita ambapo mara kwa mara mwandishi huuawa na baadaye Israel hudai kuwa alikuwa gaidi, lakini bila kutoa ushahidi wa kutosha kuunga mkono madai hayo,” alisema.

Hili si tukio la kwanza ambapo waandishi wa Al Jazeera wamelengwa na kuuawa na Jeshi la Israel kwa madai ya kuhusika na Hamas.

Mnamo Agosti mwaka jana, Ismael Al-Ghoul aliuawa katika shambulio la anga akiwa ndani ya gari lake.

Video ya kutisha iliyosambaa mitandaoni ilimuonesha akiwa amekatwa kichwa.

Mpiga picha Rami al-Rifi na mvulana mmoja aliyekuwa akipita kwa baiskeli pia waliuawa katika tukio hilo.

Katika kisa hicho, IDF ilidai kuwa Al-Ghoul alihusika katika mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel yaliyofanyika tarehe 7 Oktoba 2023 madai ambayo Al Jazeera ilikanusha vikali.

Kwa mujibu wa CPJ, waandishi wa habari 186 wamethibitishwa kuuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI