Mwanamke huyo alikuwa akisafiri kwa basi na wakati huo dereva aliona begi likisogea
Mwanamke mmoja amekamatwa nchini New Zealand akiwa na msichana wa miaka miwili kwenye begi lake. Mwanamke huyo alikuwa akisafiri kwa basi na msichana huyo akiwa ndani ya begi lake.
Kwa mujibu wa polisi, "Tukio hili lilijiri siku ya Jumapili kwenye kituo cha mabasi katika mji mdogo wa Kaiwaka kaskazini mwa New Zealand. Abiria alipomtaka dereva atoe mizigo yake, aliona begi likisogea. Dereva alipofungua begi, alikuta msichana wa miaka miwili ndani yake."
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 27 amekamatwa kwa tuhuma za unyanyasaji na uzembe kwa msichana huyo.
Vyombo vya habari vya ndani vinasema kwamba msichana huyo alifungiwa kwenye begi kwa takriban saa moja. Polisi walisema kuwa msichana huyo sasa yuko salama na mipango muhimu inafanywa ili kuhakikisha anahudumiwa .
'Mwili wa msichana ulikuwa moto'
"Mwili wa msichana ulikuwa na joto sana, lakini hakuwa na majeraha mengine," polisi walisema.
Msichana huyo amepelekwa hospitalini, ambapo anaendelea na matibabu na uchunguzi. Habari kuhusu uhusiano kati ya mwanamke na msichana haijulikani.
Mwanamke huyo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya North Shore siku ya Jumatatu, polisi walisema.
Polisi walimsifu dereva wa basi na kusema, "Tunashukuru umakini wa dereva. Alichukua hatua za haraka na kuepusha ajali kubwa."
Nini kilitokea mahakamani?
Redio ya New Zealand iliripoti kwamba mwanamke mwenye umri wa miaka 27 amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Shore Kaskazini.
Kulingana na ripoti hiyo, "Katika karatasi ya mashtaka, polisi wanasema kwamba msichana huyo huenda alikabiliwa na kukosa hewa, upungufu wa maji mwilini, uchovu wa joto na kiwewe cha kiakili. Waliita "kupunguka kwa kiwango cha kumlinda mtoto huyo".
Ikitoa taarifa kuhusu mwenendo wa kesi hiyo ndani ya mahakama hiyo, ripoti hiyo ilisema, "Mwanamke huyo hakujibu chochote mahakamani hapo, alionekana mtulivu akiwa amevalia kofia ya rangi nyepesi na kugeuza uso wake mbali na kamera. Hadi sasa hajajulikana ni nani."
Timu ya uchunguzi wa kisaikolojia itamhoji mwanamke huyo kabla ya kufikishwa tena mahakamani wiki hii.
Afisa wa polisi Simon Harrison alisema kuwa polisi wanafanya kazi kwa karibu na familia ya msichana huyo na Wizara ya Ustawi wa Watoto ya New Zealand ili kuhakikisha kwamba msichana huyo anapata usaidizi kamili na kutunzwa.
Visa kama hivyo vimeripotiwa awali
Mwaka 2016, mwanamke alisafiri kwa ndege ya Air France kutoka mjini Istanbul hadi Paris kwa kumficha msichana mdogo kwenye mkoba wake.
Shirika la ndege lilikuwa limesema kuwa msichana huyo alikuwa akisafiri bila tikiti na alikamatwa wakati wa safari ya usiku.
Chanzo cha habari cha uwanja wa ndege kiliiambia AFP kuwa mwanamke huyo ni mkazi wa Ufaransa na alikuwa katika harakati za kuasili mtoto kutoka Haiti.
Hakuruhusiwa kupanda na mtoto katika eneo la usafirishaji huko Istanbul, baada ya hapo alinunua tikiti mpya na kupanda ndege, akimficha mtoto kwenye begi.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, mwanamke huyo alimfunika mtoto kwa blanketi karibu na miguu yake katika ndege. Lakini mtoto alipolazimika kwenda chooni, abiria walimwona.
Abiria walitoa taarifa kwa wahudumu wa ndege hiyo, na baada ya hapo msichana huyo alitolewa nje ya begi.
Mnamo mwaka wa 2019, mwanamke raia wa Marekani alikamatwa nchini Ufilipino kwa mashtaka ya biashara ya binadamu baada ya kudaiwa kujaribu kusafirisha mtoto mchanga nje ya nchi.
Jennifer Talbot, 43, alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ninoy Aquino mjini Manila baada ya mamlaka kusema alikuwa akijaribu kusafirisha mtoto mchanga wa siku sita hadi Marekani kwa kumficha kwenye begi lake la kubebea.
Ofisi ya Kitaifa ya Upelelezi ya Ufilipino (NBI) kisha ilisema Talbot hakuwa ametoa taarifa zozote kuhusu mtoto huyo kwa maafisa wa uhamiaji na alikusudia kumsafirisha nje ya nchi.
Kulingana na shirika hilo, Talbott hakuweza kutoa pasi ya kusafiri ya mtoto huyo au hati yoyote. Kesi pia ilisajiliwa dhidi ya wazazi wa mtoto chini ya Sheria ya Ulinzi wa Mtoto.
0 Comments