Header Ads Widget

MLUYA WA DP AHIIDI HUDUMA BURE KWA WAJAWAZITO, MAGEUZI YA AFYA, KILIMO NA MASLAHI YA WATUMISHI


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

MGOMBEA Urais wa Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Mluya, na mgombea mwenza wake Sadous Abrahaman Khatib, wamechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, huku wakitoa ahadi kadhaa zenye lengo la kuinua maisha ya Watanzania, hususan walala hoi.

AKizungumza na waandishi mara baada ya kuchukua fomu hiyo leo Agosti 13 huku akiwa Mgombea wa 12 ameahidi ahadi zake ambapo miongoni mwa ahadi kuu za Mluya ni utoaji wa huduma bure kwa wajawazito kuanzia kipindi cha ujauzito hadi kujifungua, pamoja na malezi ya mama na mtoto kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kujifungua.

“Hakutakuwa na malipo ya kadi za kliniki, wala gharama za kujifungua Serikali itamlea mama na mtoto wake kwa miezi mitatu ya mwanzo baada ya hapo, familia itajimudu hii ni njia ya kuhakikisha uzazi salama na ustawi wa mtoto,” amesema Mluya.


Katika sekta ya afya, Mluya ameahidi pia kuwa serikali ya DP itasitisha utaratibu wa kuwatoza wananchi gharama za kuchukua miili ya marehemu hospitalini.

“Tutahakikisha familia haiwi na msiba mara mbili msiba wa kupoteza mpendwa, na msiba wa madeni. Mwili utatolewa bure kwa heshima ya marehemu ambaye alikuwa nguvu kazi ya taifa,” amesema.

Kwenye sekta ya kilimo, Mluya amesema serikali yake itahakikisha kila tone la maji ya mvua linalohifadhiwa kupitia mabwawa na marambo maalum kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, badala ya kupotea bure.

“Tutaleta kilimo cha kisasa chenye tija wakulima wataachana na jembe la mkono, walime kwa teknolojia, walime kwa biashara mazao yauzwe ndani na nje ya nchi, taifa lipate fedha za kigeni,” amesisitiza.


Miongoni mwa mambo aliyoyapinga vikali ni mfumo wa kikokotoo wa mafao ya wastaafu ambao alisema unawaumiza watumishi wa umma wanaostaafu baada ya miaka mingi ya utumishi.

“Haiwezekani mtu afanye kazi kwa miaka 34 au 35 halafu anapewa milioni 15. hii ni kuwaongezea umasikini badala ya kuwaondoa mtumishi wa serikali atapewa mkopo wa nyumba baada ya mwaka mmoja wa utumishi mzuri,” amesema.

Ameeleza kuwa hatua hiyo itapunguza vishawishi vya rushwa kwa sababu watumishi watafanya kazi kwa weledi wakijua kuwa serikali inawatambua na kuwajali.

Kwa upande wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mluya alisema askari polisi watapewa motisha kupitia maboresho ya mishahara, na wale watakaopata mikopo ya nyumba na baadaye kukutwa na hatia ya rushwa, nyumba hizo zitarejeshwa kuwa mali ya serikali au jeshi.


Katika Jeshi la Magereza, Mluya aliahidi kujenga nidhamu na heshima kwa askari kwa kuboresha mazingira ya kazi.

“Askari magereza na mfungwa hawawezi kula chakula kile kile tutajenga magereza ya kisasa yenye canteen zenye hadhi. Askari aheshimiwe,” amesisitiza.

Pia amesisitiza kuwa kesi za mahabusu zishughulikiwe kwa wakati ili kupunguza mrundikano wa watu magerezani na gharama kwa serikali.

Mluya amesema wakati umefika kwa taifa kubadili mwelekeo wa kiuongozi na kwamba DP iko tayari kusimama kwa ajili ya walala hoi.

“Saa ya ukombozi imewadia tunataka kufuta machozi ya walala hoi. Sisi DP tumekuwa mstari wa mbele kutetea haki zao,” amesisitiza.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI