Na Mwandishi Wetu.
Equity Bank Tanzania imeendeleza dhamira yake ya kukuza huduma za kifedha kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (MSEs na SMEs) kwa kudhamini Mkutano Mkuu wa Chama cha Wakandarasi Wanawake Tanzania (TWCA),hatua hii inalenga kutoa mchango wa moja kwa moja katika juhudi za kitaifa za kuwawezesha wanawake kiuchumi, hususan katika sekta ya ujenzi inayokua kwa kasi nchini.
Akizungumza katika tukio hilo, Bw. Stephen Matinya, Mkuu wa Kitengo cha Fedha za Biashara na Mtaji wa Uendeshaji wa Equity Bank, alisema benki imebuni suluhisho maalum za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wakandarasi wanawake, zikiwemo mikopo ya mtaji wa uendeshaji, ushauri wa kifedha, na huduma za kidigitali zinazorahisisha miamala,na aliongeza kuwa mipango hii inakwenda sambamba na mikakati ya maendeleo endelevu kwa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa na wanaume katika zabuni, ufadhili na fursa za biashara.
Naye Bi. Jacqueline Mollel, Meneja Mwandamizi wa Fedha za Biashara na Mtaji wa Uendeshaji, kutoka Equity alibainisha kuwa uwezeshaji wa kifedha unapaswa kuambatana na elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa miradi,na kuwa Equity Bank imekuwa ikiendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa wateja wake ili kuongeza uelewa kuhusu usimamizi wa fedha, uboreshaji wa rekodi za biashara, na matumizi ya teknolojia katika kusimamia miradi mikubwa.
Mkutano wa TWCA, uliofanyika kwa kaulimbiu “Kuwawezesha Wakandarasi Wanawake: Sera hadi Matokeo,” uliwakutanisha wadau wakubwa wa sekta ya ujenzi na miundombinu wakiwemo Wizara ya Ujenzi, Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Majadiliano yaliyoibuka yalihusu mikakati ya kutekeleza sera za usawa wa kijinsia, njia za kuongeza uwiano wa wanawake kwenye miradi ya miundombinu, na umuhimu wa taasisi za kifedha katika kutoa nyenzo za ukuaji wa biashara.
Kwa mujibu wa takwimu za CRB, wanawake wakandarasi nchini wanashiriki chini ya asilimia 15 ya miradi mikubwa ya ujenzi, changamoto kubwa zikiwa ni upatikanaji wa mitaji, vigezo vya dhamana, na ukosefu wa taarifa za soko,Equity Bank imesema inalenga kubadilisha hali hiyo kwa kutoa huduma zinazobadilika kulingana na mahitaji halisi ya wajasiriamali wanawake, ili kuongeza ushiriki wao kwenye miradi mikubwa na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.
Hatua ya kudhamini na kushiriki kikamilifu kwenye mkutano wa TWCA inachukuliwa kama kielelezo cha kujitolea kwa benki hiyo katika kuhimiza ukuaji jumuishi na ustawi wa jamii,Kwa ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi, taasisi za kifedha, na wadau wa sera, Equity Bank inaamini mazingira ya biashara yatakuwa rafiki zaidi kwa wanawake, na hivyo kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
0 Comments