Header Ads Widget

MGOMBEA URAIS WA NLD AAHIDI KUUZA MASHANGINGI YA SERIKALI KWA AJILI YA HUDUMA ZA KIJAMII


Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma 

MGOMBEA urais kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, ameahidi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atauza magari ya kifahari ya Serikali (maarufu kama mashangingi) yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200, na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya huduma za kijamii kama afya, elimu na miundombinu.

Doyo ametoa kauli hiyo leo Agosti 10, 2025, mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu,  huku akiwa mgombea wa tano ,Doyo amesema Serikali yake itakuwa ya watu na kwa ajili ya watu, akisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuboresha maisha ya Mtanzania wa kawaida.


“Nitahakikisha Serikali haitakuwa ya anasa mashangingi yote yaliyogharimu zaidi ya milioni 200 tutayauza na kuelekeza fedha hizo kuboresha huduma kama afya na elimu. Mtanzania wa kawaida lazima ajisikie kuwa sehemu ya Serikali yake,” amesema Doyo.

Akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Chausiku Khatibu Mohammed , Doyo alisema moja ya changamoto kubwa zinazowakumba wananchi ni ukosefu wa huduma bora za afya, hasa kwa wanawake wajawazito na familia zenye kipato cha chini.

“Ni aibu kwa Serikali kumdai mwanamke shilingi laki moja ili apate huduma ya kujifungua, au kudaiwa fedha baada ya ndugu yake kufariki dunia. Serikali yangu itapiga vita unyanyasaji huu wa kisera,” amesisitiza.


Katika hatua ya kuonyesha mshikamano na vijana, Doyo amefika katika ofisi za INEC kwa kutumia bajaji badala ya gari binafsi ambapo amesema bajaji ni chombo cha usafiri kinachotegemewa na vijana wengi kwa ajili ya ajira na kujikimu kimaisha.

“Nilitumia bajaji leo kwa sababu vijana wengi wanatumia chombo hiki kuendesha maisha yao. Tunatambua mchango wao, na serikali yangu itaimarisha mazingira ya ajira kwa vijana,” ameongeza.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI