Na Hamida Ramadhan, MatukioDima Media Dodoma
MGOMBEA Urais wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Mulumbe, ameahidi kuanzisha fao maalum kwa kila mzazi nchini kwa ajili ya kumlea mtoto hadi atakapofikisha umri wa miaka 18, ikiwa ni moja ya mikakati ya chama chake kuboresha ustawi wa familia.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu za kuwania urais leo Agosti 14 katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, Mulumbe amesema agizo hilo litatekelezwa ndani ya miezi mitatu baada ya kuapishwa kuwa Rais, endapo atashinda uchaguzi.
Akifafanua kuhusu vipaumbele vya serikali atakayoiunda, Mulumbe amesema elimu itakuwa bure kuanzia ngazi ya chekechea hadi chuo kikuu, na pia kufuta makato yanayokatwa kwa wahitimu kupitia Tume ya Elimu ya Juu (HELSB).
Ameongeza kuwa huduma za afya na matibabu zitakuwa bure kwa wananchi wote, akisisitiza kuwa serikali ya ADC itahakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za msingi bila gharama.
Katika sekta ya nishati, mgombea huyo ameahidi kuwa serikali yake itagharamia huduma ya kuunganishiwa umeme kwa kila mwananchi, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watumiaji wa umeme kutoka asilimia 37 ya sasa hadi kufikia asilimia 100.
Aidha, Mulumbe amesema serikali yake itanunua magari ya kuchimba visima na kuhakikisha huduma ya maji inapatikana bure kwa wananchi wote nchini.
Akizungumzia suala la miundombinu, amesema ujenzi wa barabara bora nchini utapewa kipaumbele, huku akiwashukuru wanachama wa chama hicho, makada na wananchi kwa ujumla kwa sapoti kubwa waliyoionesha hadi kufikia hatua ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya juu ya uongozi nchini.
"Tumeona maandalizi yaliyofanywa na chama tawala, lakini tuwape taarifa kwamba moto wa ADC unawaka kweli kweli hakika tunakwenda kuikabidhiwa dola kwa amani," amesema Mulumbe.
Kwa upande wake mgombea mwenza wa urais, Shoka Khamis Juma, amesema moja ya changamoto kubwa inayoyakumba vyama vya siasa ni ukosefu wa ruzuku.
Ameahidi kuwa endapo ADC itapata nafasi ya kuongoza serikali, vyama vyote vya siasa vitapatiwa ruzuku kwa kuzingatia idadi ya kura za wabunge na madiwani, si kwa kigezo cha asilimia 5 pekee kama ilivyo sasa.
Ameongeza kuwa serikali yao itaongozwa kwa misingi ya umoja wa kitaifa, ambapo kila chama kitapewa nafasi katika serikali, ili kuhakikisha mshikamano wa kitaifa na uwakilishi mpana wa kisiasa unazingatiwa.
0 Comments