Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA), Georges Gabriel Bussungu, amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akiweka wazi dhamira yake ya kuleta "mapinduzi ya njano" yanayolenga katika fikra, teknolojia, na uchumi wa kisasa unaotegemea akili mnemba (AI).
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele, Bussungu alisema Tanzania haiwezi kuendelea kubaki nyuma katika dunia ya leo ambayo inaendeshwa na teknolojia ya akili bandia.
"Ulimwengu umebadilika. Sasa ni zama za akili mnemba Artificial Intelligence. Tunahitaji si tu viongozi, bali taifa lenye fikra mnemba, ambalo linaweza kuongoza mageuzi ya kiteknolojia, kielimu, na kiuchumi kwa faida ya Watanzania wote," amesema Bussungu.
Akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Mhe. Ali Makame Issa, Bussungu ameeleza kuwa "Mapinduzi ya Njano" ni dira ya ADA-TADEA katika uchaguzi huu, yakilenga kuondoa utegemezi wa kiakili na kiuchumi, na kuandaa taifa lenye uwezo wa kushindana katika soko la dunia linalozidi kutawaliwa na teknolojia bunifu.
0 Comments