Header Ads Widget

MATUSI YAPIGWA STOP KWENYE KAMPENI ZA CHAGUZI MKUU 2025


NA MATUKIO DAIMA MEDIA,
DAR ES SALAAM.Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuhakikisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinafanyika kwa kistaarabu, bila kutumia lugha za matusi, kashfa au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza Jumatatu, Agosti 18, 2025, katika Mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), mkoani Dar es Salaam, Jaji Mutungi amesisitiza kuwa vyama vya siasa vina wajibu wa kuendeleza misingi ya amani na mshikamano wa taifa.

"Nendeni mkafanye kampeni za kistaarabu mkiwanadi wagombea wenu. Jiepusheni kabisa na lugha za matusi, kashfa, uchochezi au vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa taifa letu," amesema Jaji Mutungi.

Ameongeza kuwa amani na mshikamano ni urithi ulioachwa na waasisi wa taifa, hivyo viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi.

"Kumbukeni kuna maisha baada ya uchaguzi. Uchaguzi si mwisho wa siasa wala maendeleo. Turithishe amani hii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo," amesema.

Aidha, amewataka viongozi kutokubabaishwa na upotoshaji unaoweza kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii na makundi mengine katika jamii akisisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa.

"Mtaambiwa uchaguzi haupo, msikate tamaa. Uchaguzi upo, na jambo kubwa zaidi ni kuhakikisha tunaingia kwenye uchaguzi huru na wa haki. Ninyi ndio wakala wa kwanza wa kuhakikisha hilo linatekelezeka," amehimiza.

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI