Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Global Education Link (GEL) imewataka wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu kuwa makini na kozi wanazochagua wanapotaka kujiunga na vyyuo vikuu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Ushauri huo ulitolewa jana na Meneja Mkuu wa GEL, Regina Lema, wakati wa maonesho ya kitaaluma ya vyuo vikuu mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za sekondari zaidi ya 102 za Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema GEL imekuwa ikitoa mwongozo kwa wanafunzi mbalimbali kuhusu kozi sahihi wanazopaswa kuchukua wanapokwenda kusoma vyuo vikuu mbalimbali na kwenye maonesho hayo wametoa elimu hiyo.
Regina alisema mbali na kutoa elimu hiyo, GEL imetoa huduma za udahili wa papo kwa papo, pamoja na ushauri wa taaluma na malezi ya kitaaluma kuwawezesha wanafunzi kuelewa vyema nini cha kusomea kwa ajili ya kufanikisha malengo ya Taifa ya mwaka 2025 hadi 2050.
Regina alisema kuwa kupitia ushiriki huo, GEL pia limeimarisha uhusiano wake na shule za msingi na sekondari kwa kushirikiana na walimu na wanafunzi waliotembelea mabanda yake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, Albert Msando, alisema kuna umuhimu wa wanafunzi wakawekewa mazingira rafiki ya kuwa wabunifu na kufikiri ili hatimaye taifa liwe na kizazi chenye uwezo wa kufikiria kufanya mambo makubwa.
Maonesho hayo yaliyoandaliwa na Global Education Link (GEL), yanaendelea kwenye viwanja vya Mlimani City jijini ambapo maelfu ya wanafunzi wa shule za Dar es Salaam zinashiriki kupata mwongozo wa kusoma vyuo vikuu.
0 Comments