Header Ads Widget

MAHAKAMA KUU KUAMUA MGOGORO KESI YA MIRATHI KAKA, DADA OKTOBA 16

 

Nyumba yenye mgogoro wa mirathi awali ilikuwa Namba 10, sasa ni namba 38 iliyopo Barabara ya Singida wilayani Nzega Tabora.

NA MWANDISHI WETU, NZEGA

MAHAKAMA Kuu Masijala Ndogo ya Tabora imepanga kutoa hukumu kwenye mvutano wa dada na kaka wanaobishania usimamizi wa mirathi ya mama yao Oktoba 16 mwaka huu.

Mahakama hiyo mbele ya Jaji Dk Frank Mirindo imepanga tarehe ya hukumu baada ya pande mbili zinazopingana kuwasilisha hoja zao kwa maandishi.

Mrufani Salma Samji aliwasilisha rufani kupinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Nzega uliotupilia mbali maombi yake yakupinga kaka yake kusimamia mirathi hiyo 

Salma aliwasilisha rufani dhidi ya kaka yake, Karim Samji akiwa na hoja nne za kupinga uamuzi uliotupilia mbali maombi yake ya marejeo.

Mrufani anadai Mahakama ilikosea kisheria kukubali na kuyaunga mkono maombi namba 00007368 ya mwaka 2024 wakati Mahakama haikuelekezwa ipasavyo kufanya hivyo.

Alidai Mahakama ilikosea kisheria kukubali maombi ya kupinga yaliyowasilishwa, ilikosea kukaribisha maombi huku pande zote zikiwa hazina nguvu ya kisheria ya kushtaki kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kuwasilisha hoja hizo, mrufani aliomba rufani yake ikubaliwe na Mahakama itengue uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Nzega, maombi namba 24/2023  yaibuliwe na mlalamikiwa ashauriwe kufuata taratibu za kisheria kupinga uteuzi wa mrufani kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu mama yake.

Akijibu mjibu rufani Karim aliomba Mahakama itupilie mbali rufani na kwamba uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Nzega ulikuwa sahihi.

"Ikiwa mrufani anaamini kuwa nyumba anayotaka kusimamia pia iko chini ya usimamizi wa mlalamikiwa, basi ana njia za kisheria za kufungua shauri chini ya nafasi yake kama mwakilishi wa kisheria dhidi ya mtu yeyote akiwemo mlalamikiwa humu.

"Kuialika mahakama hii kuingia katika viatu vya mahakama iliyofanya marejeo kuamua suala kuhusu ukweli, kwa maoni yangu ni mwaliko usio na msingi ambao unapaswa kupuuzwa,"alidai Karim.

Mahakama ya Wilaya ya Nzega Machi mwaka huu ilitupilia mbali maombi ya Salma Samji aliyetaka mahakama hiyo ichunguze usahihi na uhalali wa kaka yake kuteuliwa kusimamia mirathi ya mama yao Zena Jalalkhan

Karim alidai hakuna Mahakama yoyote Tanzania iliyomteua kusimamia mali za marehemu Zainabu Jalalkhan maarufu Zena na hakuna maombi namba 35/2023 katika Mahakama ya Nyasa kuomba kusimamia mirathi ya Zainabu.

Alidai aliteuliwa kusimamia mirathi namba 35/2023 ya marehemu Zena na sio Zainabu.

Mahakama baada ya kupitia hoja za pande zote mbili iliona maombi ya marejeo yalikosa miguu ya kusimamia , muombaji alikosea kuwasilisha maombi hayo wakati aliteuliwa kusimamia mirathi ya Zainabu Jalalkhan kwenye shauri namba 24/2023.

Wanafamilia wanufaika katika mirathi hiyo ni wajukuu, Araf Seager, Aziz Seager, Haji Seager, Asha Seager, Gullam Seager, Fatuma Seager, Kasu Seager na Karim Samji ambaye ni mtoto.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI