Katika kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji madini zinafanyika kwa tija, salama na kwa kufuata viwango stahiki, kampuni ya SML kupitia tawi lake la Chunya imeendelea kutoa huduma ya upimaji wa sampuli za madini kupitia maabara za kisasa.
Akizungumza na kituo hiki Meneja wa Maabara ya Upimaji Sampuli za Madini wa SML tawi la Chunya, Hellen Shinshi, amesema maabara hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji kwani zinawawezesha kufahamu aina, wingi na ubora wa madini kabla ya kuwekeza nguvu na rasilimali kwenye uchimbaji.
"Kupima sampuli kabla ya kuanza kuchimba kwa wingi ni hatua ya msingi inayomsaidia mchimbaji kuondokana na hasara ya kutumia nguvu na fedha katika maeneo yasiyo na madini ya kutosha. Pia inahakikisha shughuli za uchimbaji zinaendeshwa kwa weledi na kwa kulinda mazingira," ameeleza Hellen.
Kwa upande wake, Misky Said Mwangomo, ambaye ni mchimbaji wa kati kutoka Chunya, amesema maabara hizo zimeleta mapinduzi makubwa kwa wachimbaji wa maeneo hayo. Amesema kupitia vipimo hivyo, sasa wanafanya maamuzi ya kitaalamu badala ya kutegemea kubahatisha kama ilivyokuwa awali.
"Awali tulikuwa tunachimba bila uhakika wa kile kilichopo chini ya ardhi. Lakini sasa kupitia huduma hizi, tunapewa taarifa kamili kuhusu madini yaliyopo – jambo linalotusaidia kuepuka hasara na kuongeza faida," amesema Misky.
Wachimbaji mkoani Mbeya, hasa katika Wilaya ya Chunya, wamekuwa wakihimizwa kutumia huduma za maabara kama njia ya kuongeza tija, kupunguza athari za kimazingira, na kuimarisha mchango wao katika pato la taifa kupitia sekta ya madini.
0 Comments